Dec 24, 2023 02:38 UTC
  • Marais wa Iran na Misri wahimiza kustawishwa uhusino wa nchi mbili katika nyuga zote

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumza kwa simu na rais mwenzake wa Misri na kutilia mkazo udharura wa kustawishwa uhusiano wa nchi hizi mbili katika nyuga tofauti.

Sayyid Ebrahim Raisi amehimiza jambo hilo katika mazungumzo yake hayo ya simu na Rais huyo wa Misri Abdel Fattah el Sisi wa Misri na kusema kuwa, kuimarishwa uhusiano wa nchi hizi mbili ni kwa manufaa pia ya Ulimwengu Kiislamu na dunia nzima kwa ujumla.

Amesema, Iran na Misri wana historia ndefu ya uhusiano wa pamoja wa kiitikadi na kihistoria na hiyo ni fursa nzuri ya kuimarishwa uhusiano wa nchi hizi mbili katika nyuga zote.

Rais Raisi amegusia pia fikra ya Imam Khomeini (MA) na kusisitiza kuwa, siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuimarisha na kunyanyua heshima ya Waislamu wote na ni za kuleta mshikamano katika safu za Waislamu; ndio maana daima Tehran inatangaza kwamba kadhia ya Palestina na haki za taifa hilo ndilo suala muhimu zaidi na la kimsingi la Ulimwengu wa Kiislamu.

Jinai zinazofanyw ana Wazayuni dhidi ya wananchi wa Ghaza hazijawahi kutokea katika historia. Kuna wajibu wa kutumia nguvu zote kukomesha jinai hizo

 

Vile vile amesema, Iran iko tayari kutumia uwezo wake wote kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Palestina hasa Ghaza na kusema kuwa, matumaini ya Tehran ni kuiona serikali ya Misri nayo inatumia uwezo wake wote kukomesha jinai za Israel na kufungua njia za kupelekewa misaada wanayohitajia wananchi wa Ghaza.

Kwa upande wake, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amepongeza siasa za Jamhuri ya Kiislamu za kuhakikisha inakuwa na uhusiano mzuri na nchi zake jirani na za ukanda huu mzima na kusema kuwa, kuna wajibu wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kuondoa vizuizi vyote vilivyopo ili kufufua uhusiano wa Misri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags