Jan 21, 2024 03:33 UTC
  • Raisi: Mauaji ya washauri wa kijeshi wa IRGC hayatapita bila kujibiwa

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amelaani vikali shambulizi la kigaidi la Israel katika mji mkuu wa Syria, Damascus lililopelekea kuuawa shahidi washauri watano wa kijeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na kusisitiza kuwa, vitendo vya aina hiyo vya kioga haviwezi kupita hivi hivi bila kupewa jibu.

Shirika la habari la IRNA limenukuu taarifa ya Rais wa Iran akieleza bayana kuwa, mauaji hayo ya kigaidi mjini Damascus yanaonesha namna utawala wa Kizayuni ulivyokata tamaa na ulivyoshindwa kukabiliana na mrengo wa muqawama katika eneo.

Amebainisha kuwa, shambulio hilo linadhihirisha namna utawala haramu wa Kizayuni umeshindwa kufikia malengo yake batili, na kwamba madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani ndio washajiishaji na wafanikishaji wa jinai hizo kwa kuendelea kuuunga mkono utawala pandikizi wa Israel.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, shambulio hilo la kigaidi kwa mara nyingine tena limetia doa kwenye rekodi za serikali zinazodai kuwa watetezi wa haki za binadamu duniani, kwa kuwa hujuma hiyo mbali na kukiuka anga ya Syria, lakini pia imekanyaga sheria za kimataifa na za ubinadamu.

Sayyid Raisi amesema hakuna shaka kuwa Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu madhubuti kwa vitendo hivyo haramu na vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa hili.

Nembo ya IRGC

IRGC imesema katika taarifa yake kwamba, washauri hao waliuawa shahidi mapema jana pamoja na idadi kadhaa ya askari wa Syria katika shambulio la Israel katika kitongoji cha Mezza mjini Damascus.

SEPAH imewataja washauri wake hao waliouawa shahidi nchini Syria kuwa ni pamoja na Hojjatollah Omidvar, Ali Aqazadeh, Hossein Mohammadi, Saeed Karimi na Mohammad Amin Samadi.

Kadhalika Rais Ebrahim Raisi wa Iran ametoa mkono wa pole kwa familia za mashahidi, uongozi na taifa zima la Iran kufuatia mauaji hayo ya kijinai yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya washauri wa kijeshi wa IRGC.

 

Tags