Amir Abdollahian: Iran imetoa ujumbe na onyo zito kwa Wamarekani
(last modified 2024-01-24T04:07:53+00:00 )
Jan 24, 2024 04:07 UTC
  • Amir Abdollahian: Iran imetoa ujumbe na onyo zito kwa Wamarekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa ujumbe na onyo zito kwa Wamarekani kwamba hatua yao ya pamoja na Waingereza katika Bahari Nyekundu dhidi ya Yemen ni kosa la kistratijia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian, ambaye yuko New York kushiriki katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Asia Magharibi, amesema kuwa: Jamhuri ya Kiislamu imetoa ujumbe mzito kwa Marekani na kutahadharisha kwamba, hatua za nchi hiyo na Uingereza za kushambulia maeneo ya Yemen ni tishio kwa amani na usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia na kupanua wigo wa vita.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema: Baada ya Marekani na Uingereza kuishambulia Yemen, picha za satelaiti zinaonyesha kuwa karibu meli 230 za biashara na mafuta zinasafirisha bidhaa katika Bahari Nyekundu; Hii ina maana kuwa wamepokea vyema ujumbe wa Wayemeni kwamba ni meli tu zinazokwenda katika bandari za utawala ghasibu wa Israel ndizo zitakazozuiliwa na Yemen.

Wiki iliyopita pia Amir Abdollahian alisisitiza katika kikao chake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Cameron pambizoni mwa kikao cha Davos nchini Uswisi kuwa, hatua ya Uingereza ya kuzidisha mizozo katika Bahari Nyekundu dhidi ya Yemen ni kosa la kistratijia.

Viongozi wa Yemen wanasema kuwa, wameamua kuzuia meli zinazoelekea kwenye bandari za Israel ili kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake dhidi ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Gaza. Badala yake, Marekani na Uingereza zimeanzisha vita dhidi ya Yemen kuunga mkono jinai za Israel badala ya kuushinikiza utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai hizo.​

Tags