Jan 31, 2024 02:45 UTC
  • Iran: US inajua ni 'suluhisho la kisiasa' tu ndilo linaloweza kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, Marekani inajua vyema kwamba ni suluhisho la kisiasa pekee ndilo linaloweza kukomesha mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kumaliza mgogoro unaoikumba Asia Magharibi.

Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa X baada ya Ikulu ya White House kuapa kwamba itatoa "jibu lenye athari kubwa" kwa shambulio la ndege zisizo na rubani lililolenga kambi ya Marekani kwenye mpaka wa Jordan na Syria.

Amir-Abdollahian amefafanua kwa kusema: "Ikulu ya White House inajua vyema kwamba suluhisho la kumaliza vita na mauaji ya kimbari huko Gaza na mzozo wa sasa katika eneo hilo ni la kisiasa. Diplomasia ndiyo ya kufanyiwa kazi katika njia hii".

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amebainisha pia kuwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu "ameshafika mwisho wa maisha yake ya kisiasa ya uhalifu".

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas kufanya operesheni ya kihistoria ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala huo haramu unaoikalia Palestina kwa mabavu kulipiza kisasi kwa hujuma na jinai za kinyama za Israel dhidi ya Wapalestina.

Netanyahu amekabiliwa na shinikizo la kujiuzulu kutokana na jinsi alivyoshughulikia vita vya Gaza na kushindwa kuwakomboa mateka wa Israel waliosalia wanaoshikiliwa katika ardhi ya Palestina.

Hata hivyo, Marekani imeendelea kuiunga mkono Israel katika vita vya Gaza ambavyo hadi sasa vimeua Wapalestina wasiopungua 26,637, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine 65,387.

Kuunga mkono Washington mauaji ya Gaza kumesababisha makundi ya Muqawama katika nchi tofauti za Asia Magharibi kuchukua hatua ya kuzilenga kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hili.

Siku ya Jumapili, harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq ilifanya shambulio la ndege zisizo na rubani kulenga kambi ya kijeshi ya Marekani ya Mnara wa 22 nchini Jordan na kuua wanajeshi watatu wa Marekani na kujeruhi makumi ya wengine.

Rais wa Marekani Joe Biden ametupia lawama kile alichokiita "makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali wanaoungwa mkono na Iran" na kuapa kuwa Washington itajibu mapigo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema haina uhusiano wowote na mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo kwa sababu mashambulio hayo yanahusu mzozo kati ya makundi ya Muqawama na jeshi la Marekani na kwamba makundi hayo yanaendesha harakati zao kwa uhuru katika operesheni zao za kuiunga mkono Palestina.../

 

Tags