Mar 27, 2024 07:40 UTC
  • Haniya: Azimio la Baraza la Usalama linaonesha Israel imetengwa duniani

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umetengwa vibaya na dunia kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa; siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio la kutaka kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza. 

Ismail Haniya alisema hayo jana Jumanne katika kikao na waandishi wa habari hapa mjini Tehran akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian na kuongeza kuwa, kupasishwa kwa azimio hilo kunaashiria kuwa utawala ghasibu unaokalia Quds tukufu kwa mabavu unashuhudia kutengwa kisiasa kusikokuwa na kifani.

Amesema ingawaje azimio hilo limechelewa na lina mapungufu, lakini kupasishwa kwake kunaonesha kuwa wananchi wa Gaza na makundi ya muqawama yamesimama kidete. Haniya ameeleza kuwa, kupasishwa kwa azimio hilo kumeweka bayana kuwa Marekani haiwezi tena kuitwisha jamii ya kimataifa ubeberu na malengo yake.

Juzi Jumatatu, wanachama 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama la UN walilipigia kura ya ndio azimilo lililowasilishwa na nchi wanachama wa kudumu wa baraza hilo kwa ajili ya kusitisha vita haraka katika Ukanda wa Gaza. Marekani ambayo ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama haikupiga kura ya turufu tofauti na nyakati zilizopita, na kwa utaratibu huo azimio la kusitisha vita Gaza likawa limepasishwa. 

Wapalestina zaidi 32,300 wameuawa shahidi na wengine elfu 74,694 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya jeshi la utawala haramu wa Israel katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba, 2023. 

Aidha Ismail Haniya amewataka Waislamu na wapenda haki kote duniani kushiriki kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Quds, ambayo huadhimishwa katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Tags