Apr 14, 2024 07:45 UTC
  • Balozi wa Iran UN: Jibu la Iran litakuwa kali zaidi iwapo Israel itaanzisha tena mashambulizi

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametangaza katika barua kwa Baraza la Usalama kwamba ikiwa utawala wa Israel utaanzisha tena mashambulizi yoyote ya kijeshi, bila shaka jibu la Iran litakuwa la nguvu na kali zaidi.

Siku 10 baada ya shambulio la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus ikiwa ni sehemu ya ardhi ya Iran na kuuawa shahidi washauri saba wa kijeshi waliokuwa nchini Syria kisheria, na baada jumuiya ya kimataifa kushindwa kujibu jinai hiyo ya kigaidi ya Israel; mapema leo Jumapili, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC)  limechukua hatua za kuuadhibu utawala huo kwa kuvurumisha ndege za kivita zisizo na rubani na makombora kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel).

Kufuatia operesheni hiyo iliyofanikiwa, Amir Saeed Iravani, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametangaza katika barua rasmi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku ikionya dhidi ya uchokozi wowote zaidi wa kijeshi wa utawala wa Israel, iko na azma isiyoyumba ya kujilinda na kutoa jibu kali kwa mujibu wa sheria za kimataifa, dhidi ya tishio au uchokozi wowote dhidi ya wananchi, mamlaka na mipaka yake yote.

Iravani amesema kwamba hatua ya kijeshi ya Iran ni utekelezaji wa haki ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kujilinda chini ya kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kujibu hujuma za kijeshi za mara kwa mara za utawala wa Israel hususan shambulio la kijeshi la utawala huo mnamo Aprili 1. Amesema shambulio hilo la Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran jijini Damascus Iilikiuka wazi kifungu cha 2 na cha 4 cha Hati ya Umoja wa Mataifa.

Kombora la Iran likiwa limetua Israel

Iravani ameongeza kuwa, kwa bahati mbaya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kutekeleza wajibu wake katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa na limeuruhusu utawala ghasibu wa Israel kukiuka misingi miekundu na misingi mikuu ya sheria za kimataifa, jambo ambalo limepelekea kushadidi taharuki Asia Magharibi.

Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni miongoni mwa wanachama wenye kuwajibika katika Umoja wa Mataifa, imejitolea kutimiza malengo na misingi iliyoorodheshwa chini ya Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa na kusisitiza msimamo wake thabiti kwamba haitaki kuongeza mivutano au migogoro katika eneo.

Tags