May 23, 2024 05:02 UTC
  • Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu asisitiza kuendelea ushirikiano kati ya Iran na Qatar

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika kikao na "Tamim bin Hamad Al-Thani" Amir wa Qatar na ujumbe aliofuatana nao, ameishukuru Qatar kwa rambirambi zake katika msiba wa kufa shahidi Sayyid Ebrahim Raisi na mashahidi wenzake, na kusisitiza haja ya kuendelea ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.

Kwa mujibu wa Kituo cha Habari cha Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jumatano katika kikao na Amir Tamim bin Hamad Al-Thani wa Qatar na ujumbe aliofuatana nao alisema ni msiba mkubwa kumpoteza rais aliyekuwa na uwezo kamili wa mambo mbali mbali kama Raisi na kuongeza kuwa:  "Pamoja na kuwa hayuko nasi tena lakini hakutakuwa na usitishajii hata kidogo wa harakati ya Iran na uhusiano  kati ya Iran na Qatar uliokuwepo wakati wa utawala wa marehemu rais utaendelezwa na  Mohammed Mokhber anayekaimu nafasi ya urais.

Akigusia hali ya eneo na juhudi za maadui za kuharibu uthabiti na amani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuwa, nchi za eneo hili zina chaguo moja tu nalo ni ushirikiano na maelewano baina yao.

"Tamim bin Hamad Al-Thani", Amir wa Qatar pia ametoa salamu za rambirambi kwa mnasaba wa kufa shahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi na wenzake, na kusema: "Uhusiano wa Iran na Qatar daima umekuwa na nguvu na njia hii itaendelea."

Wakati huo huo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwa katika kikao na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, ametoa shukurani zake kwa salamu za rambirambi za serikali na wananchi wa Lebanon kufuatia tukio chungu la kufa shahidi rais wa Iran, na akasema: "Rambirambi za umma nchini Lebanon zinaonyesha ukamilifu wa usuhuba wa nchi hizi mbili."

Mkutano wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri

Amesema Iran imempoteza mtu mashuhuri na kuongeza kuwa: Suala hili ni gumu kwetu, lakini kwa rehema za Mwenyezi Mungu, taifa la Iran litatumia tukio hilo la kusikitisha kama fursa, sawa na lilivyofanya miaka ya nyuma kwa kugeuza matukio magumu kuwa fursa."

Akigusia harakati za taifa la Iran katika mazishi ya marehemu rais na wenzake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: "Alhamdulillah, taifa letu ni taifa lililosimama na lililo macho, na imani yetu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu pia iko juu, Mwenyezi Mungu  akipenda, taifa la Iran litafaidika na tukio hili."

Ayatullah Khamenei aidha ameeleza kuridhishwa kwake na mshikamano uliopo kati ya makundi ya muqawama nchini Lebanon. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Ushiriki wa Lebanon katika masuala ya hivi karibuni ya Palestina na Gaza umekuwa na taathira kubwa, na lau jambo kama hilo halingefanyika basi Lebanon yenyewe ingepata hasara kubwa zaidi."

Katika kikao hicho, Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri pia ameeleza masikitiko ya taifa na serikali ya Lebanon kutokana na tukio la kufa shahidi Rais Raisi.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia jana jioni alikutana na Rais wa Tunisia na ujumbe aliofuatana nao ambapo alimshukuru Rais Kais Saied kwa hisia za udugu na za dhati kuhusiana na tukio la kufa shahidi rais wa Iran na wenzake na kusema: "Kumpoteza Rais na wenzake aliokuwa nalo ni jambo zito, lakini katika zama zote za uwepo wa Jamhuri ya Kiislamu, daima tumeona kwamba kwa kuzingatia hekima ya Mwenyezi Mungu na subira na istikama ya wananchi, matukio machungu yamekuwa chanzo cha maendeleo na harakati.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameeleza furaha yake kwa kuanzishwa upya uhusiano kati ya Iran na Tunisia kutokana na ziara ya Rais wa nchi hii na kuongeza kwamba: "Kuwepo shakhsia mashuhuri na wa kielimu kama Kais Saied  kama rais wa Tunisia kunaibua sura mpya na ni fursa kwa nchi hii baada ya miaka mingi ya utawala wa kimabavu na kujitenga na ulimwengu wa Kiislamu.  

Ayatullah Khamenei ameashiria harakati za watu wa Tunisia miaka michache iliyopita, ambazo zilikuja kuwa msingi wa harakati kubwa huko Kaskazini mwa Afrika na kumfahamisha Rais Kais Saied kwamba: "Wananchi wa Tunisia wana kipaji kikubwa cha maendeleo na kusonga mbele, na tunatumai kuwa kwa mpango wako  tutafikia umoja unaohitajika."

Akirejelea misimamo ya Rais wa Tunisia dhidi ya Uzayuni, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Misimamo hiyo inapaswa kuendelezwa katika ulimwengu wa Kiarabu, kwa sababu kwa bahati mbaya, katika ulimwengu wa Kiarabu, masuala hayo hayatiliwi maanani, na tunaamini kwamba njia pekee ya mafanikio ni istiqama."

Akizungumzia uwezo mzuri wa Iran na Tunisia katika kuendeleza uhusiano, Ayatullah Khamenei amesema: "Serikali ya marehemu rais wetu ilikuwa serikali ya kazi, harakati na uhusiano, na sasa Mohammad Mokhber ataendeleza njia hiyo hiyo ya kuendeleza uhusiano na nchi tofauti."

Katika mkutano huo, rais wa Tunisia Rais Kais Saied pia ametoa salamu za rambirambi za dhati za serikali na wananchi wa Tunisia kutokana na tukio hilo la kusikitisha la hivi karibuni na kusema: "Mkutano wetu wa mwisho na hayati rais wa Iran ulikuwa nchini Algeria miezi kadhaa iliyopita na huko tulikubaliana kwamba nitatembelea Tehran, lakini sikuwahi kufikiria kwamba ningekuja Tehran kutoa rambirambi zangu kwa kifo chake."

Mkutano wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Rais wa Tunisia

Akizungumzia nia ya pamoja ya nchi hizi mbili ya kupanua uhusiano katika nyanja zote, Rais wa Tunisia ameelezea matumaini yake kwamba kwa kufuata makubaliano hayo, upanuzi wa ushirikiano utafikiwa kwa njia ya kivitendo.

Kais Saied pia katika kikao hicho na Kiongozi Muadhamu ameashiria hali ya eneo na kuuawa watu wa Ghaza katika hujuma inayoendelezwa hivi sasa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kwamba: "Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuacha msimamo wake wa hivi sasa wa kutochukua hatua na badala yake kuwa na sauti moja katika kutetea haki za watu wa Palestina katika maeneo yote ya Palestina sambamba na kuundwa serikali huru ya Palestina ambayo mji wake mkuu utakuwa Quds Tukufu (Jerusalem)."

Aidha Rais wa Tunisia amebainisha kuwa: Leo hii jumuiya ya kibinadamu duniani imeipita jumuiya ya kimataifa, ambapo jumuiya ya kibinadamu katika nchi mbalimbali imejitokeza kwa sauti moja na kupinga ukatili, jinai na mauaji ya umati yanayofanywa na utawala huo wa kibaguzi huko Gaza.

Ayatollah Khamenei pia amempokea Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif ambapo ametoa shukrani zake za dhati kwa rambirambi za serikali na watu ndugu wa Pakistan.

Mkutano wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Waziri Mkuu wa Pakistan

Amesema Iran inatilia mkazo uhusiano wake na Pakistan, na inaamini katika uwezekano wa kuimarishwa uhusiano chini ya serikali mpya ya Pakistan.

Kiongozi Muadhamu amesema: "Safari ya hivi majuzi ya Raisi nchini Pakistan inaweza kuwa hatua ya mabadiliko katika uhusiano kati ya nchi hizi mbili." Kiongozi Muadhamu amesema Kaimu Rais Mohammad Mokhber ataendeleza kazi ya ushirikiano na makubaliano ya pande mbili.

Mkutano wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Waziri Mkuu wa Armenia

Sharif pia ameelezea safari ya hivi majuzi ya Raisi nchini Pakistan kuwa yenye manufaa na msingi wa upanuzi zaidi wa mahusiano na ramani ya baadaye.

Ayatullah Khamenei pia amekutana na Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan, akibainisha kuwa Tehran itaendelea kufuata sera yake ya kupanua uhusiano wake na Yerevan chini ya Kaimu Rais Mokhber.

Ayatullah Khamenei amesema marehemu Raisi alikuwa "mwenye hisia yenye nguvu"  kuhusu maswala ya mpaka yanayohusu Armenia.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Armenia amebainisha kuwa nchi yake "ilishtushwa" baada ya kusikia habari za ajali iliyomkumba rais wa Iran lakini akaeleza imani yake kwamba masuala ya Jamhuri ya Kiislamu yatashughulikiwa bila tatizo lolote chini ya maelekezo na uongozi wa Ayatullah Khamenei.

 

 

Tags