Kan’ani: Madai ya NATO ya Iran kuisaidia Russia katika vita vya Ukraine hayana msingi wowote
(last modified 2024-07-11T13:24:22+00:00 )
Jul 11, 2024 13:24 UTC
  • Kan’ani: Madai ya NATO ya Iran kuisaidia Russia katika vita vya Ukraine hayana msingi wowote

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, madai ya Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO kwamba, Iran inaisadia kijeshi Russia katika vita vya Ukraine hayana msingi wowote.

Akijibu sehemu ya taarifa ya kikao cha NATO mjini Washington, Marekani, Nasser Kanani amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayaona madai yaliyomo katika taarifa ya mwisho ya kikao cha NATO mjini Washington kuhusu msaada wa kijeshi wa Iran kwa Russia katika vita vya Ukraine kuwa hayana msingi kabisa na badala yake yana malengo ya kisiasa.

Kan’ani amebainisha kuwa, kwa bahati mbaya, tunachoshuhudia nchini Ukraine ni matokeo ya sera na vitendo vya kichochezi vya NATO zinazopigiwa upatu Marekani.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema bayana kwamba, kama tulivyokwisha sema mara nyingi, jaribio lolote la kuhusisha vita vya Ukraine na ushirikiano wa pande mbili kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia, linafanywa kwa malengo ya kisiasa kwa shabaha ya kuhalalisha uingiliaji kati na kuendeleza misaada ya silaha za Magharibi kwa Ukraine.

Viongozi wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO katika mkutano wao wa Washington

 

Nasser Kan’ani amesisitiza kuwa: Stratejia na mkakati wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima umekuwa ni jukumu la kujenga na kuleta utulivu katika njia ya kuweka usalama thabiti katika eneo na dunia kwa ujumla, na haijawahi kutoa ndege zisizo na rubani kwa Russia katika mzozo wa Ukraine na inaendelea kutilia mkazo juu ya utatuzi wa kisiasa wa mgogoro huo na kurejeshwa amani ya kudumu.

Tags