Marekani chimbuko kuu la matatizo Asia Magharibi
(last modified 2024-07-20T10:33:30+00:00 )
Jul 20, 2024 10:33 UTC
  • Marekani chimbuko kuu la matatizo Asia Magharibi

Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amekosoa vikali maamuzi na hatua za mabavu na za upande mmoja zinazochukuliwa na Marekani katika masuala mbali mbali ya Asia Magharibi na kubainisha kwamba, hatua hizo ndio chimbuko kuu la matatizo yanayolikumba eneo hili.

Ali Bagheri Kani amesema hayo huko New York Marekani alipokwenda kushiriki kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali ya mambo Palestina na Asia Magharibi kwa ujumla na kusisitiza kwamba, utendaji wa upande mmoja wa Marekani katika masuala ya kimataifa umegonga mwamba na kwamba Washington si sehemu ya suluhu, bali ni kikwazo katika mkondo wa amani duniani.

Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya CNN kwamba: Utendaji wa Marekani katika masuala ya kieneo kama vile mazungumzo ya nyuklia ya (JCPOA), uvamizi wa Wazayuni katika Ukanda wa Gaza na kadhia nyinginezo unaonyesha kuwa, Washington si tu kwamba haiwezi kuwa sehemu ya utatuzi huo, bali yenyewe ndiyo kikwazo kikuu cha kutatuliwa matatizo katika eneo hili.

Bagheri ameongeza kuwa, utendaji ghalati, wa kindumakuwili na wenye matashi ya kisiasa wa Marekani umekwamisha juhudi za kimataifa za kumaliza mgogoro wa Gaza na migogoro mingine katika eneo kama vile Afghanistan, Syria na Yemen.

 

Kwa kuzingatia mtazamo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingi za dunia zinaamini kuwa, uungaji mkono wa Marekani kwa jinai za Wazayuni na kupuuza ukandamizaji dhidi ya Wapalestina katika wakati huu unaonyesha misimamo ya kindumakuwili ya Wamagharibi dhidi ya kadhia ya Palestina na unafiki wao katika uga wa haki za binadamu.

Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Iran bado ni mwanachama wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na imejizatiti kuhuisha makubaliano hayo ya mwaka 2015 na nchi wanachama wa kundi la 5+1.

Amesema, hatua ya Marekani ya kujiondoa katika JCPOA, kwa mara nyingine ilithibitisha kutokuwa kwake mwaminifu kwa nchi na mikataba muhimu ya kieneo na kimataifa.

Kwa hakika, Marekani na tawala za Magharibi zimekuwa zikitumia kila fursa kuvuruga mchakato wa mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani. Kinyume na wajibu na majukumu yao waliyojiwekea katika mazungumzo ya nyuklia na Iran ya JCPOA hadi sasa madola hayo hayajachukua hatua yoyote ya kutekeleza ahadi zao katika uwanja huo.

Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ni makubaliano ya kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kati ya nchi za kundi la 5+1 (Marekani, Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani) ambayo yalifikiwa na Iran tarehe 14 Julai 2015 huko Vienna, Austria.

Hata hivyo, serikali ya wakati huo ya Marekani iliyokuwa ikiongozwa na Donald Trump ilichukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika makubaliano hayo Mei 8, 2018 na kuanzisha kampeni ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran. Baada ya Trump, utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani, kinyume na ahadi zake alizotoa katika kampeni za uchaguzi za kubadilisha msimamo kuhusu JCPOA, ameamua kufuata sera sawa na za utawala wa Trump. Kitendo cha Biden cha kurefusha hali ya hatari dhidi ya Iran kinaonyesha mwelekeo halisi wa Marekani dhidi ya Iran, ambao ni mwendelezo wa uadui na chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979 na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, Marekani, kama kinara wa kambi ya Magharibi, ambayo imekuwa ikijaribu kila mara kuchukua nafasi ya hegemonia (mamlaka ya amri) katika eneo la Magharibi mwa Asia, ilichukua mkondo wa kiuadui dhidi ya Iran na umeliweka suala la njama za kuupindua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni katika ajenda na sera zake.

Mkabala na hilo, Tehran imesisitiza mara kwa mara kwamba, Marekani inapaswa kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Iran kabla ya kurejea katika mapatano ya nyuklia ya  JCPOA. Vikwazo dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran vimewekwa katika hali ambayo, Marekani na tawala za Magharibi zilizopo katika JCPOA zinawajibika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mazungumzo na makubaliano ya nyuklia.

 

Kwa mujibu wa vipengee vya JCPOA, vikwazo dhidi ya Iran vinapaswa kuondolewa kuanzia siku ya kutekelezwa kwake. Hii ni katika hali ambayo, katika miaka ya hivi karibuni, serikali mbalimbali za Marekani ziliweka vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran kwa kupuuza na kutozingatia suala hilo.

Kwa hakika tajriba ya miaka 4 iliyopita imeonyesha kuwa, licha ya madai ya diplomasia ya Ikulu ya Marekani, lakini Washington haina irada na nia ya dhati inayohitajika ya kufanya uamuzi wa kurejea kwenye makubaliano ya JCPOA na kufidia sera iliyofeli ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump dhidi ya Iran.

Katika mazingira kama haya, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imesisitiza kuwa, wakati wowote pande nyingine zinapotekeleza wajibu wao kikamilifu, nayo itatekeleza kikamilifu wajibu na majukumu yake iliyojifunga nayo kwa mujibu wa makubaliano hayo ya kimataifa.

Tags