Iran: Marekani ni muungaji mkono mkuu na mshirika wa jinai za Israel
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, Marekani ndio mshirika muhimu zaidi katika jinai za kivita za utawala ghasibu wa Israel katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina na jinai zinazoendelea dhidi ya taifa la Lebanon.
Nasser Kan'ani amesema hayo katika ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X na kubainisha kwamba: Utawala wa kibaguzi wa Israel umetangaza habari ya kupokea kifurushi kipya cha msaada cha dola bilioni 8.7 kutoka kwa Marekani ili kudumisha ubora wake wa kijeshi katika eneo hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema kuwa, Washington kamwe haitabadili ahadi yake ya kuisaidia Israel "kujilinda".
Kan'ani ameeleza kuwa, ni aibu na fedheha kubwa kwamba Marekani inachukulia mauaji ya watu wapatao 42,000 katika miezi 11 huko Palestina na zaidi ya watu 1,500 katika siku 4 huko Lebanon kama "kujilinda". Kiasi hiki cha fedha si kitu kingine isipokuwa ni malipo ya mwajiri kwa wauaji.
Msemaji wa Wizara ya mashauri ya Kigeni ya Iran amesema: Walimwengu hawana shaka kwamba utawala wa Marekani ni mshirika nambari moja katika jinai za kivita za utawala ghasibu wa Israel katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina na jinai zinazoendelea dhidi ya taifa la Lebanon.
Nassir Kan'ani ameashiria jinai mpya ya Wazayuni nchini Lebanon na kueleza kuwa: Utawala wa Kizayuni uliwategea vilipuzi wajumbe ambao walitumika kwa huduma na mawasiliano; uvamizi wao huo ni kitendo cha kigaidi kilichopangwa dhidi ya mauaji ya raia wa Lebanon, na kitendo kama hicho bila shaka kinaweza kufunguliwa mashtaka ya jinai (katika mahakama za) kimataifa.