Operesheni ya Ahadi ya Kweli-2: Hatua ya Iran ya kujilinda kihalali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i117032-operesheni_ya_ahadi_ya_kweli_2_hatua_ya_iran_ya_kujilinda_kihalali
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelitaja shambulio kali la makombora la Iran la Oktoba Mosi dhidi ya utawala haramu wa Israel kuwa ni haki yake halali ya kujilinda kwa msingi wa Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa.
(last modified 2024-10-02T08:47:58+00:00 )
Oct 02, 2024 08:47 UTC
  • Operesheni ya Ahadi ya Kweli-2:  Hatua ya Iran ya kujilinda kihalali

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelitaja shambulio kali la makombora la Iran la Oktoba Mosi dhidi ya utawala haramu wa Israel kuwa ni haki yake halali ya kujilinda kwa msingi wa Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa.

Araghchi amesema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa akiashiria namna Iran ilivyoonyesha stahamala na subira kubwa kwa zaidi ya miezi miwili kufuatia jinai za mara kwa mara za utawala wa Kizayuni mjini Tehran, Ukanda wa Gaza na nchini Lebanon. Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelenga tu vituo vya kijeshi na kiusalama vya utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa: 'Licha ya kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki kuzidisha mivutano na vita katika eneo lakini wakati huo huo haiogopi vita, na kuwa iwapo utawala wa Kizayuni utajaribu kulipiza kisasi, basi jibu la Iran litakuwa kali zaidi.'

Kwa mara nyingine tena, Araghchi amezitolea wito nchi zote duniani kufanya juhudi za kusimamisha vita, kuzuia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni na kuepusha kuongezeka mivutano katika eneo hususan Lebanon na katika Ukanda wa Gaza. Amesema katika ukurasa wake wa mtandao wa X kwamba Tehran imelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya takriban miezi miwili ya kujizuia kulipiza kisasi na ili kutoa fursa ya uwezekano wa kusitishwa mapigano huko Gaza.

Amir Saeid Iravani Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, amewaandikia barua Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Pascal Chrissin Bresville, Mkuu wa Baraza la Usalama, akiwasisitizia kuwa Iran imetekeleza operesheni hiyo ya kujibu jinai za kigaidi za utawala ghasibu wa Israel katika msingi wa Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa kinachoipa kila nchi haki ya kisheria ya kujilinda na kujitetea mbele ya hujuma ya adui.

Amir Saeid Iravani Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa

Amir Saeid Iravani, ameandika katika barua yake hiyo kwamba, tofauti na ulivyo utawala wa Kizayuni ambao unaendelea kuwaua kinyama raia wasio na hatia na kuwachukulia kama shabaha halali za uchokozi wake na mauaji, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuzingatia misingi ya kimaadili na mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu na kwa kufuata kikamilifu sheria za kimataifa za kibinadamu, imelenga tu taasisi za kijeshi na kiusalama za utawala huo katika mashambulizi yake ya makombora na ikiwa ni katika hatua ya kujilinda dhidi ya uchokozi wa mara kwa mara wa utawala huo wa kibaguzi.

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baada ya miezi kadhaa ya kujizuia kuchukua hatua dhidi ya utawala wa Israel kutokana na ukiukwaji wa mamlaka yake na vitendo vya jinai vya utawala huo kufuatia mauaji ya kigaidi dhidi ya mashahidi Ismail Hania, Sayyid Hassan Nasrullah na Abbas Nilfourushan, na vile vile mauaji ya umati dhidi ya wanawake na watoto wasio na hatia wa Palestina na Lebanon, kwa kutilia maanani kifungu cha 51 cha hati ya Umoja wa Mataifa kinachozipa nchi zote haki ya kujilinda dhidi ya vitisho vya adui wa nje, Oktoba Mosi lilitekeleza Operesheni ya Ahadi ya Kweli nambari 2 ambapo lilivishambulia vituo na taasisi za kijeshi, kijasusi na kiusalama za utawala huo kwa makombora ya balistiki.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejizuia kwa muda mrefu kuuchukulia utawala wa kigaidi wa Israel hatua yoyote ya kijeshi kwa madhumuni ya kutoa fursa ya uwezekano wa kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza, na kuheshimu kikamilifu sheria za kimataifa katika uwanja huo. Lakini katika upande wa pili, ni utawala wa Kizayuni ndio umeendelea kuibua migogoro na mivutano katika eneo kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi, ambapo Iran nayo imelazimika kuchukua hatua kali na wakati muwafaka ili kuonyesha uwezo wake wa juu wa kistratijia wa kumuadhibu muhisika mkuu wa shari katika eneo, kwa msingi wa Hati ya Umoja wa Mataifa. Kutekelezwa kwa mafanikio Operesheni ya Ahadi ya Kweli nambari 2 kumetimia kwa msingi wa hati hiyo ambapo Iran imeweza kuthibitisha kivitendo kwamba inaheshimu kikamilifu sheria za kimataifa hata linapokuja suala la kujidhaminia usalama wake.