Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran apongeza nafasi ya kipekee ya Shahidi Nasrullah
(last modified 2024-10-11T11:17:34+00:00 )
Oct 11, 2024 11:17 UTC
  • Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran apongeza nafasi ya kipekee ya Shahidi Nasrullah

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuuawa shahidi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah kinyume na ulivyotarajiwa utawala wa Kizayuni wa Israel, kumeutia moyo na kuupa ari kubwa mhimili wa Muqawama katika eneo.

Hujjatul Islam wal Muslimin Kazem Seddiqi amesema hayo leo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya kimaanawi na kisiasa ya Swala ya Ijumaa hapa mjini Tehran na kueleza kwamba, kifo cha kishahidi cha Sayyid Hassan Nasrullah kimeugusa mrengo wa Muqawama, na kwamba wananchi mashujaa wa Gaza na Lebanon wamepoteza mtu ambaye alikuwa nguzo na chimbuko la kuutia moyo Muqawama.

Ayatollah Kazem Seddiqi amesema: Yeye [Shahidi Nasrullah] alikuwa mtu mwenye uzoefu na mtukufu kwa kuzingatia sifa zake za asili na uongozi wake, na alikuwa mwiba katika mwili wa maadui.

Ameongeza kwa kusema: "Suala la uenezaji wa habari na taarifa sahihi, na kwa maneno ya Kiongozi wa Mapinduzi, Jihadi ya Maelezo, ni moja ya maeneo muhimu sana ya jihadi na mapambano, na Manabii wote walianza harakati zao kutoka kwenye ngome hii."

Viongozi wa Muqawama waliouawa shahidi na Wazayuni

Kwengineko katika hotuba zake, Khatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya Pili iliyofanywa na Iran kujibu mauaji ya kigaidi viongozi wa Muqawama akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS), Ismail Haniyeh na pia Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah nchini Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah na kusema kuwa, operesheni hiyo inaonyesha kuwa jeshi la Israel halina nguvu za kukabiliana na majeshi shupavu na yenye nguvu ya Iran.

Kadhalika Ayatullah Seddiqi ameashiria hatua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kuongoza Swala ya Ijumaa Ijumaa hapa Tehran wiki iliyopita katika hali ambayo, kulikuwa na hali ya wasiwasi na taharuki na kusema kuwa, hotuba hizo za Kiongozi Muadhamu zilikuja katika wakati muafaka kwa kuzingatia kuwa, kifo cha kishahidi cha Sayyid Nasrullah kilikuwa kimewatikisa na kuwavunja moyo baadhi ya watu.

Tags