Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran yamwita balozi wa Uingereza ajieleze
Balozi wa Uingereza mjini Tehran ameitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenda kujieleza kuhusu matamshi yaliyo dhidi ya Iran yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza mjini Manama, Bahrain.
Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kutoa matamshi yaliyo dhidi ya Iran huko Manama, Bahrain, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemwita balozi wa Uingereza mjini Tehran leo Jumamosi ili kumkabidhi malalamiko ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na matamshi yasiyokubalika ya Waziri Mkuu huyo wa Uingereza.
Amesema, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya Magharibi na Ulaya amemtanabahisha balozi huyo wa Uingereza kuwa, matamshi yaliyotolewa na Bi Theresa May hayakubaliki kabisa na ni ya kichochezi na Tehran haitarajii kusikia tena maneno kama hayo kutoka kwa Waziri Mkuu huyo wa Uingereza.
Naye Nicholas Hopton, balozi wa Uingereza mjini Tehran amesema kuwa siasa za nchi yake zimesimama juu ya msingi wa kuimarisha uhusiano wake na Iran na kusisitiza kuwa, ujumbe ulio bayana na wazi wa Iran ataufikisha haraka iwezekanavyo kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo.