Uingereza, Saudia zinaituhumu Iran kuficha nafasi yao haribifu ya kuunga mkono magaidi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Matamshi dhidi ya Iran yaliyotolewa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza na Saudia Arabia ni katika njama ya kujaribu kuficha nafasi yao haribifu ya uungaji mkono magaidi wakufurishaji."
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria kikao cha pamoja na waandishi habari siku ya Jumapili baina ya Boris Johnson Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza na mwenzake wa Saudia Adel Al Jubeir mjini Riyadh na kuongeza kuwa Saudia imetenda jinai dhidi ya binadamu katika vita vyake haribifu dhidi ya watu wa Yemen.
Aidha amesema pamoja na kuwa waliowengi duniani wanalalamikia utumizi wa silaha za Uingereza katika hujuma ya Saudia nchini Yemen lakini watawala wa Uingereza wanaendelea kuiuzia Saudia silaha hizo. Amesema si tu kuwa Saudia inawahujumu watu wa Yemen kijeshi bali pia ni muungaji mkono mkuu wa ugaidi.
Msemaji wa Waizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kukaririwa madai ya Al Jubeir kuhusu uhusiano wa Iran na al Qaeda ni kichekesho na ni jambo linalotokana na ufahamu duni wa mambo.
Qassemi imesema nukta ya nguvu ya usalama wa Iran ni sera huru katika stratijia ya usalama na kutokuwa na mfungamano wowote ule na fikra za kigaidi na misimamo mikali.