Iran yataka ifidiwe baada ya Marekani kukiuka mapatano ya nyuklia
Afisa wa ngazi za juu nchini Iran amesema hatua ya Bunge la Kongresi la Marekani kuongeza kwa muda wa miaka mingine kumi Sheria ya Vikwazo Dhidi ya Iran (ISA) ni ukiukaji wa mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 na kwa msingi huo Tehran inapasa ifidiwe kutokana na ukiukaji huo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi ameyasema hayo katika mahojiano na mwandishi wa IRIB mjini Vienna, Austria jana Jumanne. Alikuwa akizungumza kabla ya kikao cha ngazi za juu cha tume ya kuratibu utekelezaji wa mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ya kundi la 5+1.
Araqchi amesema kikao cha tume hiyo kimeitishwa kufuatia ombi la Iran ili kuizuia Marekani isiendelee kukiuka mapatano hayo ya nyuklia.
Kikao hicho cha kimewaleta pamoja manaibu waziri na wakurugenzi wa kisiasa katika wizara za mambo ya nje za Iran na za nchi za 5+1 ambazo ni China, Russia, Ufaransa, Uingereza, Marekani pamoja na Ujerumani. Aidha kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Siasa katika Umoja wa Ulaya Helga Schmid.
Iran na kundi la 5+1 zilianza kutekeleza mapatano ya nyuklia ya JCPOA Januari 2016. Kwa mujiubu wa mapatano hayo, Iran iliahidi kupunguza shughuli zake za nyuklia mkabala wa kuondolewa vikwazo vinavyohusiana na nyuklia ilivyokuwa imewekewa.
Desemba mosi mwaka jana Bunge la Senate la Marekani liliidhinisha uamuzi wa Bunge la Wawakilishi kupitisha sheria ya kuiwekea Iran vikwazo kwa miaka mingine 10. Uamuzi huo ulikuwa kinyume cha mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Rais Hassan Rouhani wa Iran ameshatoa amri ya kuchukuliwa hatua za kisheria kukabiliana na ukiukaji huo wa Marekani.