Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa awasili Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i24507-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_ufaransa_awasili_tehran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amewasili mjini Tehran akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi kwa shabaha ya kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 31, 2017 07:19 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa awasili Tehran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amewasili mjini Tehran akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi kwa shabaha ya kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika safari hiyo ya siku mbili, Jean-Marc Ayrault atakutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake wa Iran, Muhammad Javad Zarif, Rais Hassan Rouhani, Spika wa Bunge Dakta Ali Larijani na vulevile Katibu Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Iran Ali Shamkhani na kujadili masuala ya kieneo na kimataifa.

Leo Jumanne Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa na mwenyeji wake, Javad Zarif watashiriki katika kikao cha kwanza cha kamisheni ya ushirikiano wa kiuchumi ya Iran na Ufaransa na kusaini hati kadhaa za maelewamo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya Ulaya na America, Majid Takhtravanchi amesema safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa mjini Tehran inafanyika katika fremu ya kudumisha mazungumzo ya mara kwa mara ya kisiasa baina ya Tehran na Paris. Vilevile Jean-Marc Ayrault atafuatilia makubaliano ya kibiashara na kiuchumi yaliyotiwa saini baina ya pande hizo mbili.

Itakumbukwa kwamba, wakati wa safari ya Rais Hassan Rouhani mjini Paris Januari mwaka jana, Iran na Ufarasna zilitia saini mikataba kadhaa ya kibiashara yenye thamani ya mabilioni ya dola.

Image Caption

Mikataba hiyo ilisainiwa baada ya makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1.

Katika kampeni zake za uchaguzi wa rais, Donald Trump, Rais wa sasa wa Marekani alitishia kufuta makubaliano hayo akiyataja kuwa ndiyo mabaya zaidi aliyowahi kushuhudia.