Rouhani: Uchumi wa Iran kustawi kwa 5%
(last modified Sun, 20 Mar 2016 15:46:08 GMT )
Mar 20, 2016 15:46 UTC
  • Rouhani: Uchumi wa Iran kustawi kwa 5%

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema nchi hii inalenga kuwa na ustawi wa kiuchumi wa asilimia tano katika mwaka mpya wa Kiirani ulioanza Machi 20.

Katika ujumbe wake huo wa Nairuzi kwa njia ya televisheni, Rais Rouhani amesema, kupitia jitihada za pamoja uchumi wa Iran unaweza kustawi kwa kiwango cha juu zaidi ya nchi zote jirani. Amesema ustawi kama huo utapelekea kuboreka uchumi na kubuniwa nafasi za ajira. Ameashiria kuwepo mkakati mpya wa serikali yake kuboresha uchumi baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani maarufu kama JCPOA.

Rais Rouhani amesema, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, taifa la Iran lilipata mafanikio makubwa ikiwemo kufikia mapatano ya nyuklia. Amesema baada ya kuondolewa vikwazo Iran sasa iko tayari kwa ajili ya harakati za kitaifa za kiuchumi.