Qassemi: Trump hajui lolote isipokuwa mafuta, dola na kudansi kwa panga
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Rais Donald Trump wa Marekani hajui lolote kuhusu dunia na eneo nyeti la Mashariki ya Kati isipokuwa fedha, mafuta na kudansi akiwa ameshika upanga.
Bahram Qassemi ambaye alikuwa akijibu maswali kuhusu hotuba iliyotolewa na Rais wa Marekani kwenye mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na hujuma yake kali dhidi ya Iran amesema kuwa: Matamshi ya Donald Trump ni ya aina yake na ya kihistoria kutokana na kotofaa kwake na kusema kuwa: Hotuba ya Rais wa sasa wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ndiyo mbaya zaidi iliyowahi kutoleawa na kiongozi wa nchi hiyo katika taasisi hiyo ya kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, Donald Trump amethibitisha kuwa ni mwanagenzi na hana maarifa ya masuala ya siasa za kigeni. Ameongeza kuwa, Rais wa Marekani ni jahili wa sheria za kimataifa na falsafa ya kuwepo Umoja wa Mataifa au anajifanya mjinga na jahili.
Bahram Qassemi amesema matamshi ya Trump yalikuwa ya kipumbavu na kijinga kiasi cha kutishia kuziangamiza nchi nyingine. Ameongeza kuwa kiongozi wa Marekani amekiuka sheria na hati za Umoja wa Mataifa kwa kujua au bila ya kujua na hajali maamuzi ya kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani ameleweshwa na ahadi za mabilioni ya fedha alizopewa na baadhi ya tawala fasidi na mbovu za eneo hili la Mashariki ya Kati kiasi kwamba alisahau kuwa anazungumza kwenye ukumbi wa Umoja wa Mataifa na mbele ya macho ya walimwengu.
Katika sehemu moja ya matamshi ya hivi karibuni kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Rais Donald Trump wa Marekani aliituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na kushambulia vikali makubaliano ya nyuklia kati ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi wanachama katika kundi la 5+1 yaliyopasishwa na Umoja wa Mataifa.