Waislamu wa Shia kote duniani waadhimisha Siku ya Tasu'a
Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameungana na Waislamu wa Kishia kote duniani katika maadhimisho ya Siku ya Tasu'a, wakifanya maombelezo ya kukumbuka mapambano ya Karbala yaliyopelekea kuuawa shahidi Imam Hussein AS.
Huku wakiwa wamevalia mavazi meusi, Waislamu katika kona zote za Iran wanahudhuria kwa wingi kwenye Husainia, Misikiti, Haram ya Imam Ridha AS, Imam wa 8 wa Waislamu wa Kishia iliyoko Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran, kama ambavyo pia wamekusanyika kwa wingi katika Haram ya Bibi Maasuma SA katika mji wa Qum, kusini mwa Tehran na katika maeneo mengine muhimu ya kidini, mitaani na majumbani kwa ajili ya maadhimisho ya Tasu'a, siku moja kabla ya kuuawa shahidi Imam wa 3 Hussein AS na wafuasi wake na askari katili wa utawala dhalimu wa Bani Umayya, mwaka 680 Hijria.
Mamilioni ya watu kadhalika wameelekea katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala ya Iraq, kwenda kushiriki kumbukizi hiyo ya tukio chungu la kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW.
Siku ya Tasu'a ambayo pia inafahamika kama 'Siku ya Mapambano' ni siku ya kumuenzi Abbas Ibn Ali, ndugu wa Imam Hussein AS kutokana na namna alivyojitolea kufa kupona katika mapambano ya Karbala.
Tarehe 10 Muharram yaani kesho Jumapili, ni siku ya Ashura, siku ya kukumbuka kuuawa shahidi mjukuu huyo wa Bwana Mtume Muhammad SAW akiwa pamoja na wafuasi wake wapatao 72, katika jangwa la Karbala, karibu karne 14 zilizopita.