Rouhani: Taifa la Iran haliwezi kusahau uvamizi wa Marekani katika eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39777-rouhani_taifa_la_iran_haliwezi_kusahau_uvamizi_wa_marekani_katika_eneo
Katika kile kinachoonekana ni radiamali kwa matamshi ya kinafiki ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katu taifa hili haliwezi kusahau vitendo vya kivamizi vya Marekani katika eneo hili la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 01, 2018 13:59 UTC
  • Rouhani: Taifa la Iran haliwezi kusahau uvamizi wa Marekani katika eneo

Katika kile kinachoonekana ni radiamali kwa matamshi ya kinafiki ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katu taifa hili haliwezi kusahau vitendo vya kivamizi vya Marekani katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Akihutuhubia umati mkubwa wa wakazi wa mji wa Sirjan, mkoani Kerman kusini mashariki mwa nchi hii leo, Rais Rouhani amepuuzilia mbali matamshi hayo ya hadaa ya Trump, ambaye alidai kuwa Washington inawaunga mkono wananchi wa Iran.

Amesisitiza kuwa, viongozi wa Washington wanafaa kuelewa kuwa, katu hawawezi kuwafanyia maamuzi yoyote wananchi watukufu wa Iran na kwamba Wairani wamekuwa wakifuatilia kwa karibu vitendo vya kivamizi vya Marekani katika eneo hili.

Dakta Rouhani amesema, "wananchi hawajasahau vitendo vyenu vya kuivamia Afghanistan na Iraq, na hii leo munaliunga mkono kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) ili kuvuruga usalama na uthabiti katika eneo."

Siku ya Jumanne, Trump katika hotuba yake ya kila mwaka mbele ya Bunge la Kongresi la nchi hiyo, kwa mara nyingine tena na baada ya kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alidai kuwa Marekani iko pamoja na watu wa Iran katika mapambano yao eti ya kupigania uhuru.

Wakazi wa Sirjan, mkoani Kerman wakimpokea Rais Rouhani

Rais wa Iran amehoji, "utasemaje una huruma na wanchi wa Iran, wakati ambapo umesimama dhidi ya Waislamu na kuwaita magaidi?"

Amekumbusha kuwa, katika enzi za dikteta Saddam Hussein wa Iraq, Marekani haikuonyesha huruma yoyote kwa Wairani wakati taifa hili lilipojikuta katika vita vya kulazimishwa vya miaka minane na Iraq.

Amebainisha kuwa, hii leo taifa la Iran limesimama kidete kuliko wakati mwingine wowote ule kulinda uhuru wake wa kujitawala, usalama na maendeleo, sambamba na kupambana dhidi ya maadui.