Troika ya Ulaya: Tutalinda makubaliano ya JCPOA bila kujali uamuzi wa Trump
Nchi tatu za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zimetoa taarifa ya pamoja na kuutangazia ulimwengu kuwa zitaendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA bila ya kujali uamuzi wa Marekani.
Jean Yves- Le Drian Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amezungumzia suala hilo la kutolewa taarifa ya pamoja ya nchi hizo tatu baada ya mazungumzo na mwenzake wa Ujerumani, Heiko Maas mjini Berlin Ujerumani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin na huku akionesha kupuuza uamuzi wowote utakaochukuliwa na rais wa Marekani, Jean Yves- Le Drian ametilia mkazo kulindwa mapatano hayo yaliyofikiwa mwaka 2015 kati ya kundi la 5+1 na Iran maarufu kwa jina la JCPOA na kueleza kuwa: Berlin, London na Paris zimedhamiria kuyalinda makubaliano hayo.
Rais Donald Trump wa Marekani anatazamiwa kuchukua uamuzi ifikapo tarehe 12 mwezi huu wa Mei kuhusu kujitoa katika makubaliano hayo au la. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wake imetangaza kuwa itachuka hatua inayofaa iwapo Marekani itajitoa katika JCPOA. Wakati huo huo ikiwa imekaribia muda ambao Trump anatazamiwa kutangaza uamuzi wake huo, pande za Ulaya zinaonekana kuzidisha jitihada zao za kuyalinda mapatano hayo ya nyuklia.