Rais wa Iran aelekea Uswisi na Austria kwa ziara rasmi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo anaanza safari rasmi ya kuzitembelea nchi za Uswisi na Austria kufuatia mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hizo mbili za bara Ulaya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Parviz Ismaili, mkuu wa idara ya habari ya ofisi ya rais wa Iran, katika safari hiyo ya siku mbili, Rais Hassan Rouhani anaongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi. Kwa mujibu wa Ismaili, katika duru ya kwanza ya safari hiyo, Rais wa Iran ataitembelea Uswisi na kukutana na Rais Alain Berset wa nchi hiyo. Katika ziara hiyo, nchi mbili zitatiliana saini mikataba kadhaa ya ushirikiano katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Akiwa nchini Austria Rais wa Iran anatazamiwa kukutana na Kansela Sebastian Kurz wa nchi hiyo na kisha nchi mbili zitatiliana saini mapatano kadhaa ya ushirikiano.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Austria. (APA), nchi hiyo imepuuza mashinikizo ya Marekani na ina azma ya kuimarisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Gazeti la Der Standard la Ausria limesema katika safari ya Rais Rouhani, Kansela Kurz anatazamiwa kusisitiza kuwa nchi yake inaunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekezwaji, JCPOA.