Abdollahian: Iran itasimama kwa nguvu zote kuwasaidia waitifaki wake
Hossein Amir-Abdollahian, msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, Iran itaendelea kusimama kwa nguvu zake zote kwa ajili ya kuwasaidia waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati.
Abdollahian ameyasema hayo katika ujumbe wake kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kusema: "Siasa zilizoshindwa za John R. Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani katika ikulu ya White House, hazitaendelea na zinamuweka pabaya Rais Donald Trump na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Israel."
Hivi karibuni na baada ya kumaliza safari yake katika utawala katili wa Israel, Bolton alikariri tuhuma dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, vikwazo na mashinikizo dhidi ya Iran vitaongezwa zaidi kwa lengo la kuilazimisha nchi hii ibadili misimamo yake.
Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza kuendelea kusimama imara dhidi ya siasa za kibeberu, ukandamizaji na uingiliaji za Marekani na waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati.