Ayatullah Amoli Larijani: Marekani imekimbia nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50394-ayatullah_amoli_larijani_marekani_imekimbia_nchini_syria
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya Marekani ya kuondoa majeshi yeke Syria na kusema kuwa, Marekani imekimbia kutoka katika nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 24, 2018 11:29 UTC
  • Ayatullah Amoli Larijani: Marekani imekimbia nchini Syria

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya Marekani ya kuondoa majeshi yeke Syria na kusema kuwa, Marekani imekimbia kutoka katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Ayatullah Sadeq Amoli Larijani amesema hayo leo katika kikao na maafisa wa ngazi za juu wa Idara ya Mahakama  hapa nchini na kubainisha kwamba, Marekani inaondoka Syria ikitoa madai ya kulishinda kundi la kigaidi la Daesh ilihali walimwengu wote wanatambua kwamba, kushindwa kundi hilo la kigaidi kumetokana na kusimama kidete wananchi, serikali halali ya Damascus, jeshi pamoja na misaada ya Iran kwa mhimili wa muqawama.

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba, subira na kusimama kidete wananchi wa Syria ndiko kulikoifanya Marekani ilazimike kuondoka katika nchi hiyo.

Wanajeshi wa Marekani nchini Syria

Ayatullah Amoli Larijani ameashiria kukaribia maadhimisho ya miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kueleza kuwa, maadui wa Iran wakiongozwa na Marekani, walifanya kila wawezalo katika kipindi cha miongo minne iliyopita ili wausambaratishe mfumo huu wa Kiislamu lakini njama zao zote hazijafua dafu.

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, licha ya kuweko njama za kila leo za maadui, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikipata uungaji mkono wa wananchi wenye uono, inaendelea kung'ara katika eneo la Mashariki ya Kati na imewapatia walimwengu tajiriba na uzoefu wa kusimama kidete na kutokubali kunyongeshwa.