IMF: Licha ya vikwazo, Iran itakuwa na akiba ya zaidi ya dola bilioni 100 mwaka huu
(last modified Sat, 04 May 2019 02:52:47 GMT )
May 04, 2019 02:52 UTC
  • IMF: Licha ya vikwazo, Iran itakuwa na akiba ya zaidi ya dola bilioni 100 mwaka huu

Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) umetabiri kuwa, akiba ya fedha za kigeni ya Iran mwaka 2019 itapindukia dola bilioni 100 licha ya kuweko vikwazo vya pande zote vya Marekani dhidi ya taifa hilo.

Katika ripoti yake ya karibuni kabisa iliyopewa jina la Malengo ya Kiuchumi ya eneo la Asia Magharibi, Afrika Kaskazini na Asia ya Kati, IMF imesema kuwa, inakadiriwa kwamba, akiba ya fedha za kigeni ya Iran mwaka huu wa 2019 itafikia dola bilioni 103 na milioni 200 na nchi hiyo itaendelea kushikilia nafasi yake ya tatu katika eneo hilo kwa kuwa na akiba kubwa zaidi ya fedha za kigeni.

Vikwazo haviwezi kamwe kuizuia Iran kufanikisha malengo yake matukufu

 

Televisheni ya CNN ya Marekani nayo imewanukuu wataalamu wa masuala ya kiuchumi na hata baadhi ya viongozi wa serikali ya Marekani na kuripoti kuwa, haiwezekani kuizuia Iran kuuza mafuta yake kwani nchi hiyo kwa kushirikiana na washitiri na wateja wake wa mafuta wana njia nyingi za kuendelea na biashara baina yao na kukwepa vikwazo.

Wiki iliyopita, serikali ya Marekani ilisema wakati wa kukaribia mwaka mmoja wa kujitoa Washington kinyume cha sheria katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran kwamba, haitoongeza muda wa msamaha kwa wanunuzi wakubwa wa mafuta ya Iran.

Mwaka 2018 pia serikali ya Marekani ilidai kuwa eti itahakikisha inaizuia kikamilifu Iran kuuza mafuta yake, lakini ilipoona ni muhali na haiwezekani kabisa kufanyika jambo hilo, iliziruhusu China, India, Japan, Korea Kusini, Uturuki, Italia na Ugiriki kuendelea kununua mafuta ya Iran. 

Tags