Zarif ajibu pendekezo la Trump la mazungumzo ya simu na Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter akijibu pendekezo la Rais Donald Trump wa Marekani la kuomba kufanya mazungumzo ya simu na wakuu wa Iran na kumfahamisha kuwa wapambe wake katika Timu B wamekuwa wakipanga njama dhidi ya Iran
Katika ujumbe wake huo wa Twitter siku ya Jumapili, Zarif amemhutubu Rais Trump na kubainisha wazi kuwa, mshauri wake wa usalama wa Taifa, John Bolton, amekuwa akipanga njama dhidi ya Iran. Zarif amemhutubu Trump kwa kusema: "Iwapo ulisahau, kabla hujamuajiri Bolton, kulikuwa na mpango aliokuwa akiupanga dhidi ya Iran akiwa na Timu B ambayo inajumuisha Bin Salman, Bin Zayed na Bibi (Benjamin Netanyahu)."
Zarif ameendelea kuandika kuwa, John Bolton ana mpango kamili wa kutoa taarifa bandia za kijasusi, vita vya kudumu na hata mpango huo unajumuisha pendekezo lisilo na maana la mazungumzo na kitu pekee ambacho hakikuwa katika mpango huo ni suala la nambari za simu.
Zarif ameambatanisha ujumbe wake huo wa Twitter na ushahidi wa mpango huo wa siri wa vita ambao umefichuliwa.
John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa Marekani amekuwa akitoa hotuba na kuandika makala zenye kuunga mkono hujuma ya kijeshi dhidi ya Iran na kupinduliwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha ni mkosoaji mkubwa wa mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA). Baada ya Bolton Kuchukua nafasi ya Mashauri wa Usalama wa Taifa, Marekani ilijiondoa katika JCPOA na kuanzisha tena vikwazo dhidi ya Iran.

Siku chache zilizopita Televisheni ya CNN ya Marekani ilitangaza kuwa Ikulu ya White House imeukabidhi Ubalozi wa Uswisi mjini Tehran, ambao unalinda maslahi ya Marekani , nambari ya simu ambayo wakuu wa Iran wanaweza kutumia kuwasiliana na Trump.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema timu "B" inayoundwa na Bolton, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na Bin Zayed mrithi wa kiti cha ufalme wa Imarati (UAE) wanajaribu kuisikuma Marekani kuanzisha vita vya kijeshi dhidi ya Iran.