Spika Larijani: Njama za Wazayuni za kuzigawanya nchi za Kiislamu zimegonga mwamba
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa pongezi na baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya ushindi wa Hizbullah ya Lebanon katika vita vya siku 33 na kusisitiza kwamba, njama za Wazayuni za kuzigawanya nchi za Kiislamu zimegonga mwamba.
Dakta Ali Larijani amesema hayo katika jumbe tofauti alizowatumia Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon na Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.
Spika wa Bunge la Iran ameashiria kushindwa utawala haramu wa Israel katika vita vya siku 33 nchini Lebanon na kueleza kwamba, ushindi huo ulitokana na ubunifu na uongozi wa harakati hiyo pamoja na nguvu ya imani, jihadi na kujitolea wapiganaji wake.
Spika Larijani amesisitiza tena juu ya himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa harakati ya muqawama mkabala na utawala dhalimu wa Israel.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria mpango wa Marekanin uliojaa njama wa "Muamala wa Karne" na kusema kuwa, mpango huo katu hautawafanya wavamizi wafikie malengo yao.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, Jumatano ya leo inasadifiana na tarehe 14 Agosti 2006 ambapo kulimalizika mapigano kati ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kutolewa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikubaliwa na pande hizo mbili.