Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran yawataka Wairani wasifanye safari nchini Ufaransa kutokana na machafuko
(last modified Wed, 11 Dec 2019 01:13:49 GMT )
Dec 11, 2019 01:13 UTC
  • Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran yawataka Wairani wasifanye safari nchini Ufaransa kutokana na machafuko

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imewataka Wairani wasifanye safari nchini Ufaransa kutokana na ghasia na migomo inayoendelea kufanyika nchini humo.

Taarifa ilitotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kuwa: Kwa kutilia maanani ghasia na maandamano yanayoendelea kufanywa na wananchi wa Ufaransa katika kipindi chote cha mwaka mmoja uliopita na kutokana na migomo ya umma ya siku mbili za karibuni na ghasia zinazoendelea katika miji mbalimbali ya Ufaransa hususan Paris, wasafiri na watalii wa Kiirani wanashauriwa kujiepusha kufanya safari nchini humo kwa ajili ya kulinda usalama wao na waahirishe safari zao hadi wakati mwingine. 

Wafaransa wanapinga sera za Emmanuel Macron

Maandamano ya migomo ya wananchi wa Ufaransa ilianza kwa shabaha ya kupinga sera za kiuchumi za Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo husuan katika nyanja za nishati na ushuru. Maandamano na upinzani huo sasa umeshika sura ya kisiasa na kupanuka zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. 

Wafaransa wanaoshiriki katika maandamano hayo yaliyopewa jina la Harakati ya Vizibao vya Njano, wanasema kuwa, sera za kiuchumi za Macron zinazidisha mbinyo na mashinikizo kwa raia na wanamtaka kiongozi huyo ang'atuke madarakani.  

Tags