"Gwaride la Huduma": Jeshi la Iran liko pamoja na wananchi katika vita dhidi ya corona
(last modified Fri, 17 Apr 2020 09:35:33 GMT )
Apr 17, 2020 09:35 UTC

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima hulinda kiwango cha uwezo wake wa kiulinzi na kumzuia adui kuanzisha mashambulizi na wakati huo huo huwa pamoja na wananchi wakati wa maafa au majanga na kuwasaidia kutatua matatizo yao.

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kila mwaka tarehe 29 Farvardin kwa kalenda ya Kiirani sawa na 17 Aprili huandaa gwaride katika maeneo yote ya Iran ya Kiislamu ambapo huonyesha mafanikio yake ya kiulinzi na kijeshi kwa mnasaba wa 'Siku ya Jeshi'. Mwaka huu, kufuatia kuibuka ugonjwa wa corona au COVID-19, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limeandaa 'Gwaride la Huduma' ambapo nara na kauli mbiu ni 'Walinzi wa Nchi na Wasaidizi wa Afya' kote katika Iran ya Kiislamu.

Katika 'Siku ya Jeshi' vifaa mbali mbali vimezinduliwa ambayvo vina umuhimu kwa mtazamo wa kijeshi na pia kwa afya ya jamii katika kukabiliana na corona. Katika gwaride mbali mbali kote Iran, Jeshi la Iran limeonyesha vifaa ya kuangamiza virusi, hospitali zinazoweza kuhamishwa, na magari ya deraya yenye vifaa vya kijeshi ambayo yanatumika katika vita dhidi ya corona.

Kufanyika gwaride na mazoezi ni jambo la kawaida katika shughuli za kila mwaka katika majeshi yote duniani na kwa msingi huo, katika 'Siku ya Jeshi', Jeshi la Iran huonyesha sehemu ndogo tu ya uwezo wake wa kujihami na kumzuia adui kuanzisha mashambulizi sambamba na kuzindua mafanikio na zana za kisasa ambazo zimeundwa hapa nchini.

Kuboreshwa uwezo wa kujihami na kivita wa Jeshi la Iran hufanyika tu kwa msingi wa kuimarisha nguvu za kumzuia adui na nguzo hii muhimu itaendelea kutekelezwa katika mazingira  na pande zote. Sambamba na kutekeleza majukumu yake ya kimsingi, Jeshi la Iran huwa pamoja na wananchi wakatika wa maafa na majanga ya ndani ya nchi. Kufanyika 'Gwaride la Huduma' katika  Siku ya Jeshi  ni mfano wa wazi wa namna Jeshi la Iran  lilivyo katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya corona na hatua hiyo ni ya aina yake  duniani.

Gwaride la Jeshi la Iran ambalo linaonyesha  kitengo cha vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19

Moja ya nukta muhimu na ya kipekee ya Jeshi la Iran likilinganishwa na majeshi mengine duniani, ni msaada wake kwa wananchi wakati wa maafa au majanga. Msingi na falsafa ya Jeshi la Iran si kuchochea vita bali ni kuchukua hatua imara na kali katika kukabiliana na tishio au hujuma yoyote ya kigeni inayolenga kukiuka mamlaka ya kujitawala na maslahi ya kitaifa ya Iran.

Kuhusiana na nukta hii, Brigedia Jenerali Kioumars Heydari kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Iran katika mahojiano na Shirika la Habari la Iran Press ameashiria msaada wa Jeshi la Iran kwa wananchi katika kipindi hiki cha kukabiliana na janga la corona na kusema: "Jeshi la Iran halichochei vita na stratijia ya pamoja na nara ya Jeshi ni kuwahudumia wananchi."

Sambamba na kuibuka ugonjwa hatari wa corona, Jeshi la Iran lilianza kutekeleza stratijia ya hujuma na kwa kutumia uwezo wake mkubwa linaendelea kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 na leo  'Gwaride la Huduma' ni misdaki ya wazi ya kutumia uwezo wote wa Jeshi la Iran katika kulinda maisha ya wananchi mkabala wa adui anayejulikana kama corona.

Afisa wa Jeshi la Iran akitoa damu katika 'Siku ya Jeshi'

Kujenga hospitali za muda na zinazoweza kuhamishwa haraka kote Iran, kuzalisha kwa wingi maski na mada za kuua virusi sambamba na kupuliza dawa za kuua virusi katika mabarabara na maeneo ya umma na hali kadhalika kuwagawia wananchi vifurushi vya afya na vyakula ni katika majukumu muhimu ya Majeshi ya Iran katika uga wa kukabiliana na corona.

Jeshi la Iran daima liko tayari kujitolea muhanga kwa ajili ya wananchi na katika zama za majanga na mfano wa hilo ni janga la sasa la corona. Aidha  katika majanga yaliyopita kama vile mafuriko na mitetemeko ya ardhi, Jeshi la Iran limekuwa pamoja na wananchi na limeonyesha kuwa si jeshi lenye kuchochea vita bali linataka amani na linawalinda wananchi kikamilifu.

Tags