Rais wa Iran aidhinisha sheria ya kukabili jinai za Israel
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameidhinisha kuwa sheria, muswada wa kukabiliana na uhasama na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika upeo wa kitaifa na kimataifa.
Rais Rouhani alipasisha sheria hiyo jana Jumanne, ambapo amezitaka taasisi zote husika za humu nchini kuhakikisha kuwa vipengee vya sheria hiyo vinatekelezwa.
Miongoni mwa taasisi hizo zilizoagizwa na Dakta Rouhani kuhakikisha kuwa sheria hiyo dhidi ya utawala wa haramu wa Israel inatekelezwa ni Wizara za Mambo ya Ndani, Intelijensia, Mashauri ya Kigeni, na Ulinzi; pamoja na Majeshi ya Iran, Baraza Kuu la Usalama la Taifa, na Idara ya Mahakama.
Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) mnamo Mei 12 ilipasisha kwa kauli moja muswada huo wa dharura wa kukabili njama za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya amani na usalama wa kieneo na kimataifa. Muswada huo ulikabidhiwa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ili kufanyiwa uchunguzi.
Kamati hiyo iliufanyia muswada huo marekebisho kabla ya kuuidhinisha na kuitwa "Muswada wa Kukabiliana na Hatua za Utawala wa Kizayuni ambazo Zinavuruga Amani na Usalama."
Sheria hiyo iliyopasishwa na Rais wa Iran inazitaka taasisi hizo za kitaifa za Jamhuri ya Kiislamu kutumia uwezo wote wa kitaifa na kimataifa kukabiliana na vitendo vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa linalodhulumiwa la Palestina na mataifa mengine ya Kiislamu ikiwemo Iran. Aidha sheria hiyo inataka kuchukuliwe hatua za kukabiliana na nafasi ya Israel katika kuvuruga usalama na amani kieneo na kimataifa.