Iran: Tutaendelea kuliunga mkono taifa la Syria, muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61685-iran_tutaendelea_kuliunga_mkono_taifa_la_syria_muqawama
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuliunga mkono na kusimama na taifa la Syria pamoja na kambi ya muqawama katika eneo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 18, 2020 12:33 UTC
  • Iran: Tutaendelea kuliunga mkono taifa la Syria, muqawama

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuliunga mkono na kusimama na taifa la Syria pamoja na kambi ya muqawama katika eneo.

Es'haq Jahangiri alisema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake ya simu na Waziri Mkuu mpya wa Syria, Hussein Arnous na kusisitiza kuwa, "mauaji ya kikatili ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani hayakubadili sera ya Iran ya kuiunga mkono Syria na kambi ya muqawama. Syria ni mshirika wa kistratajia wa Iran."

Sanjari na kulaani vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Damascus, Jahangiri amesema, "Jamhuri ya Kiislamu itafanya kila iwezalo kulipunguzia taifa la Syria mashinikizo. Kwa Rehema ya Allah, Syria itarudi katika hali yake ya kuwa na nguvu, utulivu na uthabiti."

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema mafanikio ya Syria katika vita dhidi ya ugaidi yameughadhabisha utawala wa Kizayuni wa Israel na ndiposa utawala huo haramu unaihujumu kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mpya wa Syria, Hussein Arnous amesema kuwa ushirikiano wa pande zote kati ya Damascus na Tehran umeimarisha mhimili wa muqawama dhidi ya njama za Kizayuni na Marekani katika eneo.

Sayyid Abbas Mousavi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Hivi karibuni pia, Sayyid Abbas Mousavi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema hatua ya Marekani na Umoja wa Ulaya ya kurefusha vikwazo dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu ni batili na kinyume cha sheria.

Mousavi amevitaja vikwazo hivyo kama jinai dhidi ya binadamu na ambavyo vinakiuka haki za binadamu za taifa la Syria. Hii ni baada ya EU kutangaza kurefusha vikwazo dhidi ya Syria hadi tarehe Mosi Juni mwaka 2021, kwa tuhuma kuwa eti serikali ya Damascus inakiuka haki za binaadamu.