Iran: Tunafuatilia kwa karibu nyendo za Marekani katika Ghuba ya Uajemi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Tehran inafuatilia kwa jicho la karibu nyendo na harakati za kutilia shaka za Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo Jumatatu katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, "Harakati na nyendo ghalati za Marekani katika eneo hazifichiki machoni petu."
Ameeleza bayana kuwa, "Vyombo vyetu vya kiintelijensia, usalama na jeshi vipo macho na vinafuatilia kwa karibu sana harakati za kificho na siri za Marekani katika eneo hili na Iraq."
Kauli hii ya Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ni radiamali kwa matamshi ya kichokozi na kichochezi yalitolewa jana Jumapili na Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon).
Christopher Miller, Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Marekani hapo jana alitoa amri ya kubakia katika eneo hili la Ghuba ya Uajemi manowari ya kijeshi ya Marekani iliyobeba ndege za kivita, kutokana na kile alichodai kuwa ni vitisho vya Iran dhidi ya Rais Donald Trump na maafisa wengine wa Marekani. Awali Pentagon ilikuwa imetoa agizo la kuondolewa meli hiyo ya kijeshi katika eneo la Asia Magharibi.
Alkhamisi iliyopita pia, Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuhusiana na chokochoko hizo za kijeshi zilizoanzishwa na Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi akisisitiza kwamba: Iran haitaki kuanzisha vita, lakini haitafanya ajizi katika kulinda watu wake, usalama na maslahi yake ya taifa.