Shehena ya kwanza ya chanjo ya Covid-19 ya Russia yawasili Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66468-shehena_ya_kwanza_ya_chanjo_ya_covid_19_ya_russia_yawasili_iran
Shehena ya kwanza ya chanjo ya kukabiliana na virusi vya corona ya Sputnik V ya Russia imewasili hapa nchini Iran leo Alkhamisi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 04, 2021 10:45 UTC
  • Shehena ya kwanza ya chanjo ya Covid-19 ya Russia yawasili Iran

Shehena ya kwanza ya chanjo ya kukabiliana na virusi vya corona ya Sputnik V ya Russia imewasili hapa nchini Iran leo Alkhamisi.

Shehena hiyo imewasili leo alasiri katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Imam Khomeini hapa jijini Tehran ikiwa imebeba dozi laki tano za chanjo ya Sputniv V inayozalishwa na Taasisi ya Gamaleya ya Russia. 

Balozi wa Iran mjini Moscow, Kazem Jalali amesema Russia itatuma hapa nchini Iran shehena ya pili ya chanjo hiyo katikati ya mwezi huu wa Februari, huku nyingine ikitazamiwa kuwasili hapa nchini Februari 28.

Shehena ya kwanza ya Sputnik V yawasili Iran. 

Agosti mwaka jana, Rais Vladmir Putin wa Russia alitangaza kuwa, nchi yake imetengeneza chanjo ya kwanza kabisa duniani ya virusi vya corona ya Sputnik V, huku mmoja wa mabinti zake akiwa katika watu wa kwanza kupigwa chanjo hiyo nchini Russia.

Mbali na chanjo ya COVIRAN Barekat iliyoundwa Iran kikamilifu, Iran iko mbioni kutengeneza chanjo zingine za corona ndani ya nchi na pia kwa ushirikiano na washirika wa kigeni. 

Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Iran imetangaza kuwa watu 67 wamepoteza maisha kutokana na corona ndani ya saa 24 zilizopita na hivyo kufanya idadi jumla ya walipoteza maisha hadi sasa kutokana na ugonjwa huo hapa nchini kufikia 58,256.

Aidha hadi sasa watu 1,235,581 walioambukizwa corona nchini wameweza kupona kati ya watu milioni 1,445,326 waliothibitika kuambukizwa virisi hivyo baada ya vipimo kuchukuliwa.