Iran yalaani kufunguliwa ubalozi wa Bahrain mjini Tel Aviv
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i68648-iran_yalaani_kufunguliwa_ubalozi_wa_bahrain_mjini_tel_aviv
Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, limelaani hatua ya utawala wa kifalme wa Bahrain kufungua ubalozi katika utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 04, 2021 07:55 UTC
  • Iran yalaani kufunguliwa ubalozi wa Bahrain mjini Tel Aviv

Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, limelaani hatua ya utawala wa kifalme wa Bahrain kufungua ubalozi katika utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa ya makao makuu ya kongamano hilo imesema watawala wa Bahrain hawataweza kuunusuru utawala wa Kizayuni wa Israel ambao uko katika mkondo usioepukika wa kusambaratika. Taarifa hiyo imesema hatua hiyo ya Bahrain inaenda kinyume na matakwa ya Wabahrain pamoja na Waislamu kote duniani.

Aidha taarifa hiyo imesisitiza kuwa Palestina, ni ardhi inayokaliwa kwa mabavu na Israel na kwamba mji mtakatifu wa Quds ulio katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu ni milki ya Wapalestina. Taarifa hiyo imeongeza kuwa mji wa Quds ni qibla cha kwanza cha Waislamu na ni kitovu cha mitume na mahala ambapo Mtume Muhammad SAW alipaa na kuelekea mbinguni.

Sehemu ya mji wa Quds uliko Msikiti wa Al Aqsa

Taarifa ya Makao Mkauu ya Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina katika Bunge la Iran imeashiria mapambano ya miongo saba ya Wapalestina dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel ambao pia ni maarufu  kwa kuua watoto na kusema, hatimaye Wapalestina wataweza kukomboa ardhi zote zinazokaliwa kwa mambavu na kwamba njama zozote za usaliti hazitavunja azma na irada ya Wapalestina na waitifaki wao.

Hali kadhalika taarifa hiyo imetoa wito kwa mabunge yote kuunga mkono taifa la Palestina katika mapambano dhidi ya hujuma za utawala wa Kizayuni kwa kulaani hatua zozote za kuanzisha uhusiano na utawala huo dhalimu.

Hivi karibuni Bahrain ilitangaza rasmi kufungua ubalozi wake Tel Aviv baada ya pande hizo mbili kufikia mapatano ya kuanzisha uhusiano mwezi Septemba mwaka jana.

Katika dikrii ya Machi 30, Mfalme wa Bahrain Hamad Bin Isa Aal-Khalifa alitangaza kuanzisha ubalozi wa ufalme huo huko Israel na akamteua Khalid Yusuf Al-Jalahma kuwa balozi wake.