Iran: Chokochoko za Wazayuni haziwezi kuachwa zipite vivi hivi bila ya majibu
Katibu Mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina amesisitiza kuwa, chokochoko za Wazayuni haziwezi kuachwa zipite vivi hivi bila ya majibu.
Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Alkhamisi wakati alipoonana na Nasser Abu Sharif, mwakilishi wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina hapa Tehran na kuongeza kuwa, kambi ya muqawama itaendelea kutoa majibu makali kwa Wazayuni kutokana na chokochoko zao.
Vile vile ameashiria matukio ya eneo hili, Palestina na Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo itakuwa Ijumaa ijayo ya mwisho ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kusisitiza kuwa, maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ilianzishwa kwa ubunifu wa Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yatazidi kuyaamsha mataifa yanayopenda haki dunia na kuyaongezea nguvu za kukabiliana na dhulma, ukandamizaji na uvamizi wa aina yoyote ile.
Aidha amesisitiza kuwa, matokeo ya ujuba na kiburi cha utawala wa Kizayuni yatakuwa ni kupata kipigo kikali zaidi kuliko ilivyopata huko nyuma.
Katibu Mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina pia amesema, uungaji mkono wa pande zote kwa kambi ya muqawama na kuweko mshikamano wa nchi za Kiislamu ndiyo njia bora ya ushindi usiopingika dhidi ya wavamizi wa Quds.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jihadul Islami ya Palestina hapa mjini Tehran ameishukuru Jamhuri ya Kisilamu ya Iran kwa uungaji mkono wake wa pande zote kwa taifa linalodhulumiwa la Palestina na kusema kuwa, nguvu bandia na za kipropaganda za utawala wa Kizayuni wa Israel zimezidi kuonekana ndani ya utawala huo katika matukio ya wiki iliyopita.