Iran: Kinga ya kutoshitakiwa viongozi wa Israel barani Ulaya haipaswi kuendelea
Ofisi ya Uwakilishi ya Iran katika Umoja wa Ulaya imetuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kusema kuwa, kinga ya kutoshitakiwa viongozi wa Israel wanaotenda jinai kubwa za kinyama dhidi ya watu wasio na hatia, haipaswi kuachiwa iendelee.
Ofisi hiyo imesema, kitendo cha nchi za Magharibi cha kunyamazia kimya jinai za utawala wa Kizayuni hakileti sura nzuri hata kidogo na imesema, kinga ya kutoshitakiwa Israel barani Ulaya inabidi ifutwe.
Ofisi hiyo pia imeandika, mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel huko Ghaza yameua zaidi ya watoto wadogo 60 wasio na hatia. Imesema hizo ni jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu ambazo zimefanywa na Israel kwa kiwango kikubwa kisichokanushika.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait amesema kuwa, jinai za kutisha za jeshi la utawala wa Kizayuni huko Ghaza ni jinai ya kivita.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Ahmed Nasser Mohammed al Sabah alisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, msimamo wa nchi yake ni kuendelea kuiunga mkono Palestina hadi wananchi wake waweze kukomboa ardhi zao na kupata haki zao zote zilizoghusubiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesema, Palestina inabidi iwe nchi huru kwenye mipaka ya mwaka 1967 na mji mkuu wake lazima uwe ni Baytul Muqaddas.
Kuanzia tarehe 10 mwezi huu wa Mei utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanya mashambulizi makubwa ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Ghaza huko Palestina kwa muda wa siku 12 na kufanya uharibifu mkubwa sambamba na kuua na kujeruhi idadi kubwa ya Wapalestina wasio na hatia.