Khatibzadeh: Kuikaribisha Israel eneo la Ghuba ya Uajemi kunavuruga amani
-
Saeed Khatibzadeh
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema kuwa, aina yoyote ya kuandaa mazingira ya kuwepo Israel katika eneo la Ghuba ya Uajemi inatazidisha machafuko na mivutano katika eneo hilo na kunapaswa kulaaniwa.
Saeed Khatibzadeh ambaye mapema leo alikuwa akizungumzia safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala haramu wa Israel, Yair Lapid huko nchini Bahrain amekumbusha hatua ya kudhalilisha ya watawala wa Bahrain ya kutangaza waziwazi uhusiano wao na utawala huo ghasibu na kusema kuwa, mapokeza ya kujidhalilisha na kujikomba ya watawala hao kwa afisa huyo wa utawala unaoikalia Quds kwa mabavu ni kinyume na matakwa ya wananchi sharifu na wapenda uhuru wa Bahrain.
Khatibzadeh ameeleza kusikitishwa na hatua ya serikali ya Bahrain ya kupuuza na kufumbia macho jinai na uhalifu unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina na akasema, hatua kama hizo haziwezi kuhalalisha uwepo wa utawala huo haramu na wala hazitaathira mapambano ya kupigania ukombozi wa Quds tukufu na kibla cha kwanza cha Waislamu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesisitiza kuwa doa hilo la fedheha halitafutika katika kipaji cha nyuso cha viongozi wa Bahran na kuongeza kuwa, watu wa eneo hilo la Magharibi mwa Asia wanapinga sera za kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.