Mazungumzo ya Vienna; anga nzuri ndani ya kivuli cha ubunifu wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80322-mazungumzo_ya_vienna_anga_nzuri_ndani_ya_kivuli_cha_ubunifu_wa_iran
Awamu ya nane ya mazungumzo ya Vienna baina ya Iran na kundi la 4+1 inaendelea katika Hoteli ya Palais Coburg nchini Austria huku kukiwa na dalili nzuri za kufanyika mazungumzo katika mazingira yenye kuleta matumaini. Mazungumzo hayo yanaendelea baada ya kusimama kidogo kwa ajili ya kutoa fursa kwa timu za mazungumzo kurejea katika nchi zao kwa mashauriano.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Feb 13, 2022 23:41 UTC
  • Mazungumzo ya Vienna; anga nzuri ndani ya kivuli cha ubunifu wa Iran

Awamu ya nane ya mazungumzo ya Vienna baina ya Iran na kundi la 4+1 inaendelea katika Hoteli ya Palais Coburg nchini Austria huku kukiwa na dalili nzuri za kufanyika mazungumzo katika mazingira yenye kuleta matumaini. Mazungumzo hayo yanaendelea baada ya kusimama kidogo kwa ajili ya kutoa fursa kwa timu za mazungumzo kurejea katika nchi zao kwa mashauriano.

Timu ya mazungumzo ya Iran imetoa mapendekezo mapya katika awamu hii ya nane ya mazungumzo ya Vienna na wakati huo huo imezihamasisha pande nyingine nazo zitoe mapendekezo na ubunifu wao. Hatua hiyo inaonesha ni kiasi gani Tehran imeingia kwenye mazungumzo hayo ikiwa na muelekeo wa wazi na madhubuti. Mahdi Safari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya udiplomasia wa kiuchumi naye amejiunga na timu ya Iran katika mazungumzo ya kutafuta njia za kuondolewa Tehran vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa.

Kiujumla ni jambo la dharura kabisa kuweko wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Iran katika mazungumzo hayo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina na wa kiutaalamu zaidi kwa shabaha ya kufikia kwenye makubaliano ya kuondolewa vikwazo hivyo. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana kukawa kuna mshikamano na mashauriano ya mtawalia baina ya pande zote zinazohusika na mazungumzo hayo. Kushiriki kwa kauli moja timu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna ni ushahidi mwingine wa jinsi Tehran ilivyo na nia ya kweli ya kufikia makubaliano ya maana katika mazungumzo hayo licha ya kwamba kuna ishara za wazi zinazoonesha migongano baina ya misimamo ya ujumbe wa Marekani mjini Vienna na siasa za ndani ya nchi hiyo. 

 

Zaidi ya hayo ni kwamba, baadhi ya pande za mazungumzo ya Vienna zinaacha kujishughulisha na masuala ya mazungumzo na zinashughulishwa zaidi na kuuridhisha utawala wa Kizayuni. Inavyotegemewa kwa baadhi ya tawala za Magharibi ni kutangaza haraka misimamo na maamuzi yao ili kuharakisha kufikiwa mapatano katika mazungumzo ya Vienna na zisicheleweshe mambo kwa ajili ya kuiridhisha Israel.

Muda wote utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya uharibifu katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Kila baada ya muda utawala huo pandikizi huwa unatoa madai ya kipuuuzi na yasiyo na mashiko ili kuzuia kufikiwa mapatano mapya ya kuondolewa vikwazo Iran. Huko nyuma yaani mwaka 2015, aliyekuwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu alizusha mambo mbalimbali ya kipuuzi ili kuyapiga vita mapatano ya JCPOA lakini alishindwa kuzuia kufikiwa makubaliano hayo ya kimataifa. Hivi sasa pia utawala wa Kizayuni wa Israel umeanzisha wimbi jipya la njama zake baada ya kuona ishara nzuri za kufikiwa makubaliano ya kuondolewa Iran vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa.

Kwa kuzingatia kuwa hivi sasa anga ya mazungumzo ya Vienna ni nzuri na inatia matumaini, kitu ambacho kitazidi kuzifanya pande za mazungumzo kuwa karibu na makubaliano ya mwisho, ni nia ya kweli na kuchukuliwa maamuzi yanayotakiwa ya kisiasa na baadhi ya pande zinazoshiriki kwenye mazungumzo hayo.

Wang Qun, mwakilishi wa China katika mazungumzo ya Vienna

 

Wang Qun mwakilishi wa China katika mazungumzo ya Vienna alisema juzi Jumamosi kwamba: Pande zote za mazungumzo zina misimamo inayofanana. Mazungumzo ya Vienna yameshaingia kwenye hatua yake ya mwisho hususan baada ya Iran kuwasilisha kifurushi cha mwisho cha mapendekezo yake.

Msimamo huo wa China umetangazwa katika hali ambayo afisa mmoja wa ngazi za juu wa Iran huko Vienna ameliambia shirika la habari la Iran Press kwamba: Kubadilishana mapendekezo pande zinazozungumza ni jambo la kawaida kabisa, na tangu mwanzoni kabisa mwa mazungumzo haya, Iran imeshatoa mapendekezo mengi kwa pande nyingine za mazungumzo.

Tumalizie uchambuzi huu wa kisiasa kwa kusema kuwa, wajibu wa kulindwa matunda ya mradi wa amani wa nyuklia wa Iran ambao umefanikiwa kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na jitihada za wanasayansi vijana wa Iran, kuna daraja sawa na wajibu wa kuondolewa vikwazo vyote ilivyowekewa kidhulma Iran. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia masuala yote hayo mawili kwa daraja sawa katika mazungumzo ya Vienna.