Iran yaipongeza Afrika Kusini kwa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82544-iran_yaipongeza_afrika_kusini_kwa_kuwaunga_mkono_wananchi_wa_palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameipongeza Afrika Kusini kwa misimamo yake ya kuwaunga mkono na kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 15, 2022 07:39 UTC
  • Iran yaipongeza Afrika Kusini kwa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameipongeza Afrika Kusini kwa misimamo yake ya kuwaunga mkono na kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina.

Katika mazungumzo yake na simu na mwenzake wa Afrika Kusini jana Alkhamisi, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hilo la kusini mwa Afrika linadiriki na kufahamu masaibu ya wananchi wa Palestina kwa kuwa lenyewe lilikumbwa na mfumo wa ubaguzi wa apartheid.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini hivi karibuni ilisema kuwa, historia ya utawala wa zamani wa ubaguzi wa rangi nchini humo (apartheid) inalilazimisha taifa hilo la kusini mwa Afrika kuwa sauti ya wanaodhulumiwa na kutelekezwa katika kona mbalimbali za dunia wakiwemo Wapalestina.

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  amesema kuwa, Tehran iko tayari kuimarisha na kustawisha uhusiano wake na Afrika Kusini katika nyuga mbalimbali. Amesisitiza kuwa, suala la kuimarishwa uhusiano wa Iran na nchi za bara la Afrika hususan Afrika Kusini litafuatiliwa kwa umakini mkubwa kwa ajili ya maslahi ya pamoja ya mataifa yote.

Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amepongeza mielekeo ya pamoja ya Jamhuri ya Kiislamu na Afrika Kusini katika kuyaunga mkono mashirika ya kimataifa na kusisitiza kuwa, nchi mbili hizi zitaendelea kufungamana na mkondo huo.

Waafrika Kusini daima wamekuwa wakiwaunga mkono wananchi wa Palestina mkabala wa Israel

Kwa upande wake, Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu kwa kuiunga mkono nchi hiyo ya Kiafrika katika taasisi na mashirika ya kimataifa na kusisitiza kuwa, Afrika Kusini inaitambua Palestina kama taifa rafiki.

Hali kadhalika Bi Pandor ameamualika Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuitembelea Afrika Kusini na kueleza kuwa, anatumai safari hiyo itaandaa mazingira ya kuimarika zaidi uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Pretoria.