Iran na Mauritania zahimiza kuimarisha ushirikiano wao katika nyuga zote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82712-iran_na_mauritania_zahimiza_kuimarisha_ushirikiano_wao_katika_nyuga_zote
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Mauritania na kutilia mkazo udharura wa kuimarishwa uhusiano wa Tehran na Nouakchott katika nyuga zote.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Apr 20, 2022 07:48 UTC
  • Iran na Mauritania zahimiza kuimarisha ushirikiano wao katika nyuga zote

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Mauritania na kutilia mkazo udharura wa kuimarishwa uhusiano wa Tehran na Nouakchott katika nyuga zote.

Mazungumzo hayo ya simu yamefanyika usiku wa kuamkia leo Jumatano ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian amemuombea dua za Ramadhani waziri mwenzake wa Mauritania, Mohamed Salem Ould Marzouk na kumpongeza kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania akisema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatilia mkazo kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano wa nchi hizi mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amesema, kuimarishwa uhusiano wa Tehran na nchi za Afrika ni katika vipaumbele vikubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, juhudi za Tehran za kuimarisha uhusiano wake na nchi za magharibi na kaskazini mwa Afrika zinafanyika kwa lengo hilo hilo.

Bendera za Iran na Mauritania

 

Amir-Abdollahian pia amezungumzia matatizo mbalimbali ya umma wa Kiislamu na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefurahishwa na hatua ya kusimamishwa vita nchini Yemen na ina matumaini kuwa usimamishaji huo utakuwa wa kudumu kwa kutilia mkazo kuondolewa vikwazo vyote walivyowekewa wananchi wa Yemen kama vile kuzingirwa na wavamizi wa nchi hiyo kutokea angani, baharini na ardhini.

Kwa upande wake, waziri mpya wa mambo ya nje wa Mauritania, Mohamed Salem Ould Marzouk amekaribisha juhudi za Iran za kuimarisha uhusiano wa pande zote na nchi yake na ameishukuru Tehran kwa msimamo wake wa kutotetereka wa kutetea wanyonge wakiwemo wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.