Kiongozi: Mazungumzo ya nyuklia yamethibitisha Marekani haina mwamana
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Tunapaswa kutumia uzoefu wa mazungumzo ya nyuklia yaliyothibitisha kuwa Marekani haina mwamana na hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ichukue mkondo wake wa ustawi.
Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo hapa mjini Tehran katika mjumuiko mkubwa wa watu wa matabaka mbalimbali kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyoaga dunia Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yapata miaka 27 iliyopita.
Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuhusu kufuata msingi wa kimapinduzi wa Imam Khomeini na kusema, hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza nchi kustawi na kufikia malengo ya wananchi na ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilitoka katika udhibiti wa madola ya kibeberu na kuwa na mfumo wa Kiislamu ambao ni kigezo cha kuigwa na mataifa mengine. Kiongozi Muadhamu amesema, Imam Khomeini kwa misimamo yake ya Kimapinduzi aliweza kuiokoa Iran kutoka katika kinamasi cha utegemezi, ufisadi wa kisiasa na kimaadili, udhalilishaji wa kimataifa na kubakia nyuma kielimu, kiuchumi na kiteknolojia.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, Imam Khomeini, alielekeza reli ya harakati ya Iran upande wa ufanikishaji wa malengo makubwa yaani, 'Utawala wa Dini ya Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa, Dini ya Mwenyezi Mungu inajumuisha kupatikana uadilifu wa kijamii kwa maana yake halilisi, kung'oa mizizi ya umasikini na ujinga, kuondoa matatizo ya kijamii, kuhakikisha nchi inastawi kielimu, inatumia uwezo wake, sambamba na kupata izza na utambulisho wa kitaifa na nguvu za kimataifa.
Kiongozi Muadhamu amesema Mapinduzi ya Kiislamu ni rasilimali ya kipekee ya taifa la Iran na kuongeza kuwa Mapinduzi yalipatkaana kwa gharama kubwa lakini pamoja na hayo yalikuwa na faida nyingi sana.
Ayatullah Khamenei ameashiria kuendelea kuwa imara Mapinduzi ya Kiislamu baada ya miaka 37 ya ushindi wake na kuongeza kuwa, leo hali ya taifa la Iran iko wazi zaidi ya huko nyuma.
Kiongozi Muadhamu halikadhalika amesema uchumi wa kimapambano ndio njia pekee ya kuweza Iran kujitegemea kiuchumi.
Ayatullah Khamenei ameashiria uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani kwa nchi ambayo inawashambulia watu wa Yemen na kusema, Marekani ni mshirika katika mauaji ya watu wasio na hatia huko Yemen. Kiongozi Muadhamu amesema, kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu haipaswi kunyamazia kimya jinai hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel, sawa na Uingereza na Marekani ni adui wa taifa la Iran. Ametoa wito wa kuchukuliwa tahadahri kuhusu kila pendekezo linalotolewa na adui hasa mapendekezo ya kisiasa na kiuchumi.