Raisi: Azimio la IAEA dhidi ya Iran lilitia doa muamana wa kisiasa
Rais wa Iran amesema azimio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) lilikuwa na taathira hasi kwa muamana na irada ya kisiasa ya pande husika.
Rais Ebrahim Raisi wa Iran alisema hayo jana Jumamosi katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kueleza kuwa, lengo la kupasishwa kwa azimio hilo ni kutaka kuliweka chini ya mashinikizo taifa la Iran.
Azimio hilo lilipendekezwa na Marekani pamoja na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na lilipasishwa mwezi uliopita wa Juni na Bodi ya Magavana ya IAEA licha ya upinzani mkali wa China na Russia.
Sayyid Ebrahim Raisi amezikosoa vikali nchi hizo za Magharibi zilizoandaa rasimu ya azimio hilo, kutokana na misimamo na mienendo yao haribifu.
Amesema anaitakidi kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa iwapo masuala yenye utata yatapatiwa ufumbuzi, sanjari na kutoa dhamana upande wa pili wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Rais Raisi ameashiria nafasi athirifu ya Iran katika kulinda na kudhamini usalama wa eneo la Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, matatizo ya nchi za eneo yanapaswa kupatiwa ufumbuzi na mataifa na serikali za eneo, na si kwa uingiliaji wa madola ajinabi.
Kadhalika amelaani vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, vikwazo hivyo havijawa na taathira hasi kwa taifa hili tu, bali kwa uchumi wa dunia na hususan chumi za Ulaya.
Aidha Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kusaidia kuhitimisha vita vya Ukraine, na kutatua matatizo yaliyopo kupitia mazungumzo ya kisiasa.
Kwa upande wake, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mbali na kupongeza msimamo wa Iran wa kupinga hatua za kijeshi za madola fulani ya eneo nchini Syria, amebainisha kuwa Paris itaendeleza jitihada za kuhakikisha kuwa mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA yanazaa matunda.