Gharibabadi: Magharibi inatumia suala la wanawake kuzishinikiza nchi huru
Afisa wa ngazi ya juu wa haki za binadamu nchini Iran amesema nchi za Magharibi zinatumia suala la wanawake kuziweka chini ya mashinikizo nchi huru duniani.
Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Kibinadamu la Iran, Kazem Gharibabadi amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Namizata Sangare, Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Haki za Binadamu la Ivory Coast.
Sangare ni miongoni mwa shakhsia waliokuja hapa Tehran kwa ajili ya kushiriki katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Wanawake Wenye Ushawishi. Aidha wanawake wenye taathira kutoka mataifa ya Senegal, Nigeria, Burkina Faso, Guinea Conakry, Cameroon na Guinea Bissau walihudhuria mkutano huo.
Gharibabadi amesisitiza kuwa, Wamagharibi hawana ustahiki wa kuzungumzia suala la haki za binadamu kutokana na namna wanavyokiuka kwa wingi haki za binadamu katika kona mbalimbali za dunia.
Ameeleza bayana kuwa, kukanyaga haki za binadamu za watu huru ni sehemu ya sera ya nje ya akthari ya nchi za Magharibi zinazodai kuwa ni vinara wa kutetea haki za binadamu.
Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Kibinadamu la Iran amebainisha kuwa, taifa la Iran lipo chini ya vikwazo shadidi vya upande mmoja, na iwapo nchi za Wamagharibi zingelikuwa zinajali kweli haki za Wairani wakiwemo wanawake na watoto, basi zingeliachana na uraibu wao wa vikwazo.
Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Wanawake Wenye Taathira lilifanyika hapa mjini Tehran Ijumaa iliyopita na kuhudhuriwa na wanawake 300 kutoka nchi 96 duniani katika mabara matano duniani wakiwemo wake za marais wa zamani wa Niger, Sri Lanka, Guinea na mke wa Waziri Mkuu wa Armenia.
Kwa upande wake, Namizata Sangare, Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Haki za Binadamu la Ivory Coast ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuandaa mkutano huo wa aina yake. Amesema kongamano hilo limeweka wazi nafasi muhimu ya wanawake wa Iran katika ngazi za familia, jamii na siasa.