Jebeli: Kuweza Muqawama wa Palestina kuushurutisha utawala wa Kizayuni ni ushindi mkubwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i98194-jebeli_kuweza_muqawama_wa_palestina_kuushurutisha_utawala_wa_kizayuni_ni_ushindi_mkubwa
Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) ameyapongeza makundi ya muqawama ya Palestina kwa ushindi wao mkubwa katika mapigano ya hivi karibuni na utawala haramu wa Kizayuni wa Israe ambayo yalimalizika tu baada ya Israel kukubali masharti yao.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
May 30, 2023 03:10 UTC
  • Jebeli: Kuweza Muqawama wa Palestina kuushurutisha utawala wa Kizayuni ni ushindi mkubwa

Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) ameyapongeza makundi ya muqawama ya Palestina kwa ushindi wao mkubwa katika mapigano ya hivi karibuni na utawala haramu wa Kizayuni wa Israe ambayo yalimalizika tu baada ya Israel kukubali masharti yao.

Peyman Jebeli ameyasema hayo katika mkutano na Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina Ziyad al-Nakhalah mjini Beirut, Lebanon.

Jebeli amebainisha kuwa makundi ya muqawama ya Palestina kufanikiwa kuweka masharti yao ya usitishaji vita dhidi ya utawala wa Kizayuni ni ushindi mkubwa, wa kudumu na wa kupigiwa mfano.

Mkuu wa IRIB alikuwa akizungumzia makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya makundi ya Wapalestina yenye makao yao katika Ukanda wa Gaza na utawala haramu wa Israel kufuatia siku tano za mashambulio ya kinyama ya utawala huo katika eneo hilo la pwani. Mapigano hayo yalishuhudia ufyatuaji wa wimbi kubwa la makombora yenye nguvu ya harakati ya Jihadul-Islami dhidi ya vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni na miji mingine katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na kufika hadi Tel Aviv.

Mkuu wa IRIB Dkt Peyman Jebeli

Kutokana na jibu kali lililotolewa na Muqawama wa Palestina, hatimaye utawala ghasibu wa Israel ulilazimika kusalimu amri kwa masharti yao kabla ya kufikiwa usitishaji vita, ikiwa ni pamoja na ahadi ya kusimamisha mauaji ya viongozi wa Muqawama.

Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu wa Jihadul-Islami amesema katika kila vita na utawala wa Kizayuni, muqawama wa Palestina umepata uungaji mkono mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

“Linganisha tu [hali yetu] miaka 20 au 30 iliyopita na leo. Tulikuwa vipi wakati huo na tukoje hivi sasa? Haya yote [yamewezekana] kupitia uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu kwa Muqawama wa Palestina," amesema Ziyad al-Nakhalah.

Mkuu wa IRIB ambaye aliwasili Beirut, mji mkuu wa Lebanon, siku ya Ijumaa kwa ziara maalumu nchini humo hadi hadi sasa ameshakutana na viongozi mbalimbali wa nchi hiyo akiwemo Katibu Mkuu wa harakati ya muqawama ya Hizbullah Sayyed Hassan Nasrallah, Spika wa Bunge Nabih Berri na Waziri wa Utamaduni wa nchi hiyo Mohammad Wissam al-Murtada.../