Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; Adui Mzayuni amechanganyikiwa
Akizungumza karibuni na Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina na ujumbe aliofuatana nao, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema hali ya sasa ya utawala wa Kizayuni wa Israel inatofautiana sana na ya miaka sabini iliyopita na kusisitiza: Hii leo adui Mzayuni yuko katika hali ya kutojua la kufanya na hali hii inaonyesha kuwa Jihad Islami ya Palestina na makundi mengine ya mapambano yametambua vyema njia ya kufuata na yanasonga mbele kwa busara.
Akizungumza siku ya Jumatano katika kikao na Ziad al-Nakhaleh Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, na ujumbe aliofuatana nao, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ametoa pongezi kwa harakati hiyo kwa ushindi wa vita vya hivi karibuni vya Ghaza na kusisitiza kuwa, harakati hiyo na makundi mengine ya mapambano ya Kiislamu yamepata ufunguo halisi wa kupambana na utawala wa Kizayuni. Ameongeza kuwa: "Kuongezeka kila siku nguvu ya makundi ya mapambano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni ufunguo halisi wa kumpigisha magoti adui Mzayuni, na njia hii inapasa kudumishwa."
Matamshi hayo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu yanaweza kuchukuliwa kuwa yanaashiria matukio ya karibuni ambayo yanathibitisha wazi kudhoofika utawala wa Kizayuni ambao umekuwa ukizikalia kwa mabavu na kwa miongo kadhaa ardhi za Wapalestina na kutekeleza huko jinai za kutisha. Hivi sasa mizozo ya ndani, mipasuko ya kisiasa na ishara za kusambaratika utawala wa Kizayuni kwa upande mmoja, na kuongezeka silaha za makundi ya mapambano pamoja na uungaji mkono wa kimataifa kwa ajili ya kutetea haki za watu wa Palestina kwa upande wa pili, kumeongeza maradufu matumaini ya kuangamizwa utawala huo bandia na kukombolewa Quds Tukufu.
Maandamano makubwa ya mitaani katika miezi ya hivi karibuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kwa lengo la kupinga mageuzi ya mahakama yanayofuatiliwa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, kuongezeka mivutano katika bunge, Knesset, kutokuwa na uwezo wa kuunda baraza imara la mawaziri, kutokuwa na imani wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na viongozi wao wa kisiasa na kukimbia Wazayuni kutoka Israel ni mifano michache tu ya matatizo ya ndani ambayo yanaukabili utawala huo unaoukalia kwa mabavu Quds Tukufu.
Katika uga wa kieneo na kimataifa, utawala wa Kizayuni unakabiliwa na hali ngumu kwani baada ya miaka 75 ya juhudi za Wazayuni na waungaji mkono wao hususan Marekani kwa ajili ya kuudhaminia nafasi nzuri katika eneo, hivi sasa utawala huo umepoteza itibari katika ngazi za kimataifa kuliko wakati mwingine wowote. Maandamano ya umma yanayofanyika katika pembe tofauti za dunia, ikiwemo Marekani, katika Siku ya Kimataifa ya Quds na kutangazwa uungaji mkono kwa wananchi wa Palestina ni thibitisho la wazi la ukweli kwamba utawala wa Kizayuni unaendelea kupoteza itibari kimataifa.
Wakati huo huo, kupungua ushawishi wa Marekani katika eneo ikiwa mshirika mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni na kuimarika muunganiko wa nchi za Kiislamu pia kunaonyesha kuwa matukio ya eneo hili yanaenda kinyume na matakwa ya utawala wa Kizayuni.
Nukta nyingine muhimu ambayo imeashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni suala la kuongezeka nguvu ya makundi ya mapambano ya Kiislamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, jambo ambalo bila shaka linaweza kuupigisha magoti utawala huo ghasibu unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu. Hivi sasa wanamapambano wa Palestina huko Gaza na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na vile vile nchi za Kiislamu, wote wanazidi kuimarisha umoja wao kuliko ilivyokuwa huko nyuma, ambapo ushindi wa karibuni wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina katika vita vya siku 5 dhidi ya hujuma ya kinyama ya utawala huo unathibitisha wazi ukweli huo.
Mei 9 mwaka huu, jeshi la Kizayuni lilianzisha operesheni mpya ya kinyama iliyoitwa "Ngao na Mshale" dhidi ya Ukanda wa Gaza, ambayo ilidumu kwa muda wa siku tano. Katika siku ya pili ya hujuma hiyo, chumba cha pamoja cha makundi ya mapambano ya Palestina nacho kilitangaza kuanzisha operesheni ya "Tha'r al-Ahrar" (kisasi cha walio huru) ambapo utawala huo ulikabiliwa na jibu kali la mamia ya maroketi na makombora kutoka kwa wanamapambano wa Kiislamu.
Ijapokuwa utawala wa Kizayuni ulitaka kuiangamiza Jihad Islami na kuharibu uwezo wake wa makombora katika vita hivyo, lakini harakati hiyo ya mapambano ya Palestina ilirusha takriban maroketi na makombora 1,500 katika maeneo ya adui Mzayuni katika vita hivyo na hivyo kudhihirisha wazi kuimarika nguvu zake za kijeshi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
Ayatullah Khamenei amesema kuhusiana na hilo: "Jihad ya Kiislamu ya Palestina imeonyesha mafanikio makubwa katika vita vya hivi karibuni vya Ghaza, na hivi sasa hali ya utawala wa Kizayuni imebadilika ikilinganishwa na miaka sabini iliyopita, ambapo viongozi wa Kizayuni wana haki ya kubabaika kutokana na wasiwasi wa kutoona kutimia miaka themanini ya utawala huo."