Iran: Utawala wa Kizayuni unapanda upepo, ujue utavuna kimbunga
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusu mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Palestina kwamba, jinai za utawala huo dhalimu na uhalifu wake unazidi kuipunguzia uhai Israel katika ramani ya dunia.
Nasser Kan'ani Chafi ameandika hayo kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na huku akigusia muqawama wa kishujaa wa wananchi madhlumu wa Palestina mbele ya jinai na unyama mkubwa wa utawala wa Kizayuni amesema, anayepanda upepo ajue atavuna kimbunga.
Ameongeza kuwa, muqawama ni majibu ya kawaida na ya haki ya taifa la Palestina mbele ya ugaidi, kuporwa ardhi zao, ubaguzi na unyama wa kuchupa mipaka linaofanyiwa na utawala katili wa Israel.
Amesisitiza kuwa, ugaidi wa kitaasisi na uhalifu wa kiserikali wa Wazayuni hautoachwa vivi hivi bila ya kupata majibu yanayostahiki.
Jeshi la utawala wa Kizayuni kwa kushirikiana na shirika la kijasusi na usalama wa ndani la Shin Bet la Israel limefanya jinai ya kuwaua wanamapambano watatu wa Palestina kwa kutumia ndege isiyo na rubani yaani droni, huko Jenin, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Wanamuqawama hao wa Palestina wameuliwa shahidi, kidhulma na kigaidi na wanajeshi wa Israel wakati wakiwa kwenye gari.
Brigedi za Jenin zenye mfungamano na Saraya al Quds, tawi la kijeshi la Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina zimetoa taarifa na kusema kuwa, wanamapambano wake watatu wameuliwa shahidi na droni ya utawala wa Kizayuni. Makundi mbalimbali ya muqawama ya Palestina yamelaani vikali jinai hiyo ya Wazayuni.
Hazim Qassem, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, kuwaua kigaidi vijana wa Palestina kwa kutumia jeshi la adui Mzayuni na kwa kutumia droni, ni kitu ambacho hakiwezi kuachwa vivi hivi bila ya kupata majibu makali kutoka kwa taifa shujaa la Palestina.