Marais wa Iran na Russia wazungumzia uasi wa Wagner, masuala ya Caucasia
Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono mamlaka ya kujitawala Russia na vile vile hatua zilizochukuliwa na serikali ya Moscow kukomesha uasi wa kundi la Wagner wa Juni 24.
Rais Raisi amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Rais wa Russia, Vladimir Putin na kuongeza kuwa, masuala ya Caucasia yanapasa kupatiwa ufumbuzi na nchi za eneo hilo pekee bila uingiliaji wa maajinabi.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Sayyid Raisi akisema, "Tunafuatilia masuala ya eneo la Caucasia kwa makini, na tunaamini kuwa mizozo katika eneo la Caucasia inapaswa kufumbuliwa na nchi za eneo hilo."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, uwepo wa vikosi vya kigeni katika eneo ni tishio kwa usalama na uthabiti wa nchi na mataifa ya eneo hili la kistratajia.
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin amemfahamisha Rais wa Iran juu ya uasi wa hivi karibuni nchini Russia na kueleza kuwa, Moscow ilichukua hatua za makusudi kuzima uasi huo.
Mohammad Jamshidi, Naibu Afisa Mkuu katika Ofisi ya Rais wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema, marais wa Iran na Russia katika mazungumzo hayo ya jana Jumatatu walikaribisha mazungumzo ya amani baina ya Armenia na Azerbaijan ya kujaribu kutatua mvutano juu ya eneo la Karabakh linalogombaniwa na nchi mbili hizo za Kusini mwa Caucasia.
Aidha amesema marais wa Iran na Russia wamejadiliana kuhusu kadhia ya mchakato wa amani nchini Syria, mbali na uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Moscow, masuala ya kieneo na kimataifa.