Iran: Mapatano ya amani na Israel hayawezi kukomesha ukatili wa utawala huo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali mashambulizi ya jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa mji wa Jenin, huko kaskazini mwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu.
Kanali ya Press TV imemnukuu Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akisema hayo jana Jumatatu na kusisitiza kwamba, kufikia mapatano ya amani na utawala haramu wa Israel kamwe hakuwezi kuuzuia utawala huo kuendeleza ukatili na jinai zake dhidi ya Wapalestina madhulumu.
Kan'ani amesema hayo baada ya jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kufanya mashambulizi ya kinyama kwenye kambi ya wakimbizi ya Jenin katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, na kuua shahidi Wapalestina wasiopungua wanane na kujeruhi makumi ya wengine.
Mashuhuda wamevieleza vyombo vya habari kuwa jeshi la utawala dhalimu wa Israel limefanya mashambulizi 10 ya anga mjini Jenin usiku wa kuamkia jana na kusababisha moshi kufuka kutoka kwenye mabaki ya majengo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza bayana kuwa, "Tukio hilo la kusikitisha, linalojumuisha mashambulizi ya makombora ya angani na ardhini yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya jiji la Jenin, ni kitendo cha kijinai, na mfano wa wazi wa ugaidi wa kiserikali."
Nasser Kan'ani amebainisha kuwa, mapatano yoyote ya amani na Israel hayawezi kusimamisha ukatili wa utawala huo, kwani jinai ni dhati na sehemu ya sera na mfumo wa utawala huo pandikizi.