Mar 12, 2024 05:54 UTC
  • Kushadidi mivutano baina ya vyama vya upinzani na Baraza la Mawaziri la Israel

Yair Lapid, kiongozi wa chama cha upinzani cha Yesh Atid amekiri juu kushadidi hitilafu na mizozo ya ndani baina ya vyama vya upinzani na Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Yair Lapid, kiongozi wa upinzani dhidi ya Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel amesema kuwa, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo amepoteza imani ya nusu ya Baraza la Mawaziri na wananchi waliowengi. Matamshi ya Lapid ambaye chama chake kinahesabiwa kuwa chama kikubwa zaidi kinacholipinga Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni katika Bunge la Israel (Knesset) ni kiashirio cha wazi cha kushadidi tofauti kati ya Netanyahu na vyama vya upinzani. Yair Lapid, kiongozi wa chama cha Yesh Atid, chama muhimu zaidi cha upinzani cha muungano wa Likud katika Bunge la Israel (Knesset) anachukuliwa kuwa mpinzani mkuu wa Netanyahu.

Kauli hizo mpya za Lapid zinakuja wakati ambao mivutano ya kisiasa huko Tel-Aviv imefikia katika  kilele chake. Baraza la Mawaziri la Netanyahu kivitendo halijafanikiwa katika vita vya Gaza, na kushindwa mtawalia kwa jeshi la Kizayuni kumeiweka rehani nafasi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu pamoja na Baraza lake la Mawazri ambalosasa linaonekana kukalia kuti kavu.

Tofauti kati ya Netanyahu na vyama vya upinzani zinahusiana na kutumwa Wayahudi wa Kiharedi (Wazayuni wa Orthodox) kama vikosi vya kijeshi kwenye vita huko Gaza. Kidhahiri Wazayuni wa Orthodox hawaonekani kuwa na harakati za  kisiasa, lakini ndio mada kuu ya mzozo kati ya baraza la mawaziri la Kizayuni na mrengo wa upinzani.

Yair Lapid

 

Lapid na washirika wake wa kisiasa wanataka kupelekwa Wazayuni wa Orthodox vitani, vinginevyo haki zao zinapaswa kukatwa na kuusitishwa. Lakini mkabala na hilo, Netanyahu na Wazayuni wenye misimamo ya kufurutuu ada katika Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wanapinga kupelekwa vitani Wazayuni wa Kiorthodox.

Ili kuepuka kufanyika kwa uchaguzi wa mapema, Netanyahu hana budi kudumisha uungaji mkono wake kwa Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada, kwani kuendelea kwa hitilafu hizo kutapelekea kusambaratika kwa baraza la mawaziri na hivyo kuitishwa uchaguzi wa mapema. Kwa hakika hilo linaonekana kuwa jambo linalotarajiwa. Lakini suala kuu ni kuwepo kwa Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada, kama Itamar Ben-Gvir, waziri mwenye itikadi kali wa usalama wa ndani na  Bezalel Yoel Smotrich Waziri wa Fedha wa utawala wa Kizayuni katika baraza la mawaziri, ambao wanapinga vikali kutumwa vitani Wazayuni wa Kiorthodox.

Matokeo ya kuongezeka kwa hitilafu na mivutano  kati ya Netanyahu na Lapid yatapelekea kufanyika uchaguzi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel. Matokeo ya uchunguzi wa maoni yanaonyesha kuwa, endapo uchaguzi utafanyika leo, mungano wa Likud utashindwa, na wakati huo huo vyama vya upinzani vitaweza kufikia makubaliano ya kuunda Baraza la Bawaziri lakini kwa tabu na mashaka makubwa.

Mivutano ya ndani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu inaongezeka kila siku, katika hali ambayo, kutoridhika na suala la kuendelea kwa vita vya Gaza pia kumesababisha kuibuka maandamano ya kila siku dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

 

Netanyahu alikuwa ameahidi kuhitimisha haraka vita na kudhibiti Gaza kwa muda mfupi tu na kuisambaratisha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS). Lakini katika mazingira ya leo, si yeye tu na walio karibu naye ambao wameshindwa kufikia malengo yao, bali jeshi la utawala wa Kizayuni nalo limekabiliwa na vipigo na kushindwa mtawalia mbele ya makundi ya muqawama ya Palestina. Fauka ya hayo, hata uungaji mkono wa Marekani kwa Israel nao haujazaa matunda.

Matukio yanayoshuhudiwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) yatakuwa mwendelezo wa duru mpya ya ukosefu wa utulivu na maelewano ya ndani ambayo Baraza la Mawaziri la Netanyahu na Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada na vyama vya upinzani wakiwemo wafuasi wa Lapid walikuwa na mchango mkubwa katika kuundwa kwake na wakapigia upatu kwa shabaha ya kusukuma mbele gurudumu la malengo ya kisiasa.

Tags