Mar 14, 2024 06:37 UTC
  • Hali mbaya ya mateka wa Kipalestina katika jela za Kizayuni

Katika taarifa yake, Klabu ya Mateka wa Palestina imetahadharisha kuhusu hali mbaya ya mateka hao wanaoshikiliwa katika jela za utawala wa kibaguzi wa Israel.

Kabla ya kuanza vita vya Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023, idadi ya mateka wa Kipalestina katika jela za Kizayuni ilikuwa karibu 5,000. Idadi ya mateka hao imeongezeka mara mbili katika kipindi cha miezi 5 iliyopita, ya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza. Kwa mujibu wa tangazo la klabu hiyo ya mateka wa Palestina, Wapalestina 9100 (wakiwemo watoto na wanawake) wanashikiliwa katika jela za kutisha na zenye hali mbaya sana za utawala wa huo ghasibu wa Kizayuni.

Mbali na mauaji ya kimbari huko Ghaza, utawala  wa Israel pia umezidisha ukatili wake dhidi ya wafungwa wa Kipalestina. Suala hili pia limeashiriwa katika taarifa ya klabu hiyo ya mateka na wafungwa wa Palestina. Inaeleza kuwa tangu kuanza kwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, idara ya magereza ya Israel imezidisha mateso dhidi ya wafungwa wa Kipalestina.

Mateka na wafungwa katika jela za Wazayuni

Moja ya jinai zinazotekelezwa na utawala unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu dhidi ya wafungwa wa Kipalestina ni kuwanyima chakula na kuwaweka njaa. Kwa hakika siasa za kuwaweka njaa wafungwa na mateka sambamba na kuwatesa wakiwemo wanawake na watoto ni miongoni mwa siasa chafu zinazotekelezwa na utawala ghasibu wa Al-Quds tangu tarehe 7 Oktoba. Hali hiyo imewasababishia mateka na wafungwa hao matatizo makubwa ya kimwili, hasa katika mfumo wao wa kusaga chakula.

Kamati ya Masuala ya Mateka na Walioachwa Huru (inayofungamana na Mamlaka ya Ndani ya Palestina) hivi karibuni ilionya kuhusiana na sera za kuwaweka njaa wafungwa wa Kipalestina, ambazo zinaendeshwa na utawala wa Kizayuni katika jela zake. Huku ikiashiria kikao cha wanasheria wake na idadi kadhaa ya wafungwa wa Kipalestina, kamati hiyo imetangaza kuwa, wafungwa wa Kipalestina katika jela za Kizayuni kwa wastani wamepungua uzito wa kati ya kilo 15 hadi 25.

Suala jingine ni kwamba chakula kidogo wanachopewa wafungwa hakitayarishwi katika mazingira masafi. Mbinu zisizo sahihi za utayarishaji na utumiaji chakula zinaifanya miili ya wafungwa hao kukumbwa kirahisi na virusi na magonjwa mbalimbali. Kuhusiana na suala hilo, na kwa mujibu wa ripoti za kuaminika, idadi ya wafungwa wagonjwa imeongezeka, na tangu Oktoba 7 njaa bado inatumiwa kama chombo cha kuwaadhibu mateka na wafungwa katika jela hizo.

Askari wa Kizayuni wakiwakamata watoto wa Kipalestina

Aidha Idara ya magereza ya Kizayuni inakataa kutibu na kuwapa dawa wafungwa wanaougua. Kamati inayoshughulikia Masuala ya Wafungwa wa Kipalestina na inayofungamana  na Mamlaka ya Ndani ya Palestina imesisitiza kuhusu suala hilo kuwa kunyimwa dawa na matibabu wafungwa wagonjwa katika msimu wa baridi kali mwaka huu kumeathiri sana afya zao, ambapo utawala huo vamizi hata haukuruhusu wafungwa hao wapelekewe nguo zinazofaa za kujikinga na baridi.

Suala jingine ni kuwa, licha ya hali mbaya ya kiafya inayowakabili wafungwa hao, utawala wa Kizayuni pia umewanyima haki zao za kidini. Sambamba na kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani, utawala wa Kizayuni umewazuia wafungwa wa Kipalestina kutekeleza majukumu yao ya kidini katika jela hizo za kuogofya.

 

Tags